Harry Kane hashikiki, Bayern moto hauzimi Bundesliga
Muktasari:
- Kane, mwenye umri wa miaka 32, sasa ana mabao 18 katika mechi 10 za Bayern msimu huu, na wiki iliyopita alifikisha rekodi ya kuwa mchezaji wa kasi zaidi karne hii kufikia mabao 100 akiwa na klabu moja katika ligi kuu tano bora Ulaya.
HARRY Kane ameendeleza rekodi yake ya mabao baada ya kufunga tena huku Bayern Munich ikiichapa Eintracht Frankfurt mabao 0-3 na kuendeleza mwanzo bora kwenye Bundesliga msimu huu, ikipanua uongozi kileleni kwa pointi nne.
Kane, mwenye umri wa miaka 32, sasa ana mabao 18 katika mechi 10 za Bayern msimu huu, na wiki iliyopita alifikisha rekodi ya kuwa mchezaji wa kasi zaidi karne hii kufikia mabao 100 akiwa na klabu moja katika ligi kuu tano bora Ulaya.
Katika mechi iliyochezwa Jumamosi Oktoba 4, 2025 kwenye Uwanja wa Deustche Bank Park, nahodha huyo wa Uingereza alitengeneza historia nyingine kwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao 11 katika mechi sita za kwanza za Bundesliga, akipiga shuti la chini kutoka mbali lililoipa Bayern bao la pili katika kipindi cha kwanza.
Luis Díaz alifunga mara mbili, na kuhakikisha kikosi cha Vincent Kompany kinapata ushindi, huku ikitumia nafasi ya Borussia Dortmund iliyotoka sare ya 1-1 dhidi ya RB Leipzig mapema siku hiyo.
Bayern na Dortmund zinatarajiwa kukutana kwenye mechi ijayo mara tu baada ya mapumziko ya kimataifa.
Mabao ya Bayern yalianza mapema ambapo sekunde ya 15 tu Díaz alimalizia krosi ya Serge Gnabry, likiwa ndilo bao la mapema zaidi msimu huu katika Bundesliga.
Kane alifunga bao lililokataliwa kwa kuotea, huku kikosi cha Dino Toppmöller kikidhani kimerejea mchezoni baada ya Jean-Matteo Bahoya kufunga bao zuri, lakini VAR ililibatilisha baada ya kubaini kulikuwa na handball kutoka kwa Ritsu Doan kabla ya kufungwa bao hilo.
Kane alitulia na kuongeza bao la pili dakika ya 27 lililowapa Bayern utulivu kabla ya kipindi cha mapumziko, na baadaye alipiga mwamba kipindi cha pili.
Ulinzi wa Bayern ulihimili shinikizo la Frankfurt, waliokuwa wamefunga mabao 17 katika mechi zao tano za kwanza, kabla ya Díaz kukamilisha ushindi huo kwa kufunga bao lake la pili dakika ya 84 na kuhakikisha Bayern inapata ushindi wao wa 10 mfululizo tangu kuanza msimu wa 2025–2026.
Hata hivyo, kulikuwa na hofu kidogo baada ya Kane kutolewa uwanjani dakika za mwisho kutokana na kuumia kifundo cha mguu.
“Niko kwenye hatua ya kupona kwa sasa,” amesema Kane baada ya mechi hiyo wakiwa ugenini.
“Nimepata pigo kidogo tu. Nitapumzika kwa siku chache na nitakuwa sawa, hakuna tatizo kwa timu ya taifa. Nitakuwepo Jumatatu.”
Uingereza itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Wales Alhamisi kwenye Uwanja wa Wembley kabla ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Latvia mjini Riga, Oktoba 14, 2025.
MATOKEO BUNDESLIGA OKTOBA 4, 2025
Augsburg 3-1 Wolfsburg
Leverkusen 2-0 Union Berlin
Dortmund 1-1 RB Leipzig
Werder Bremen 1-0 St. Pauli
Frankfurt 0-3 Bayern