Habari njema kwa Simba, Berkane yapata pigo
Muktasari:
- Klabu hiyo imethibitisha kutokuwepo kwa nyota huyo katika taarifa ya kitabibu iliyotolewa kufuatia jeraha alilopata katika mechi dhidi ya Hassania Agadir, uliokuwa sehemu ya raundi ya saba ya Ligi Kuu ya Morocco.
RABAT, Morocco: HABARI njema kwa Simba ni wapinzani wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika, RS Berkane ya Morocco kupata pigo baada ya winga wake, Mounir Chouiar kuumia nyama za paja na kutarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa takribani wiki nne.
Klabu hiyo imethibitisha kutokuwepo kwa nyota huyo katika taarifa ya kitabibu iliyotolewa kufuatia jeraha alilopata katika mechi dhidi ya Hassania Agadir, uliokuwa sehemu ya raundi ya saba ya Ligi Kuu ya Morocco.
Kutokana na majeraha hayo Chouiar ataikosa mechi ya kwanza Kundi C ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Simba itakayofanyika Morocco kati ya Novemba 27-29.
Uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa Chouiar amepata majeraha ya kuchanika kwa misuli ya nyuma ya paja. Kwa mujibu wa taarifa ya RS Berkane, mchezaji huyo anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa takribani wiki nne huku akiendelea kufuatiliwa na madaktari wakati wa matibabu na kurejea kwake katika hali nzuri.
Klabu hiyo inayotumia rangi ya machungwa imeeleza kuwa itaendelea kufuatilia maendeleo ya afya ya mchezaji huyo na namna anavyoitikia matibabu anayopatiwa.
RS Berkane imemtakia Chouiar kupona haraka na kueleza matumaini yake ya kumuona akirejea kikosini akiwa katika hali nzuri zaidi.