Pedro anusurika kutimuliwa AS Far
Muktasari:
- Uongozi wa klabu hiyo unaelezwa kuendelea kuwa na imani na kocha huyo raia wa Ureno, ukiamini anahitaji muda zaidi wa kurekebisha mwenendo wa timu na kurejesha ushindani.
RABAT, Morocco: UONGOZI wa klabu ya AS FAR ya Morocco haujafikiria kumtimua kocha wake mkuu, Pedro Goncalves, licha ya timu hiyo kupitia kipindi kigumu cha matokeo, huku ukitarajiwa kuendelea kumpa nafasi hadi baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
Uongozi wa klabu hiyo unaelezwa kuendelea kuwa na imani na kocha huyo raia wa Ureno, ukiamini anahitaji muda zaidi wa kurekebisha mwenendo wa timu na kurejesha ushindani.
Kwa sasa, AS FAR inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi sita, matokeo ambayo hayajaufanya uongozi kufikiria mabadiliko ya haraka katika benchi la ufundi.
Klabu hiyo inaamini kuwa kuna sababu mbalimbali zilizoathiri kiwango cha timu, ikiwamo majeraha ya wachezaji kadhaa pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo wachezaji wapya katika kuzoea mfumo na mazingira ya kikosi. Kutokana na hali hiyo, uongozi unapendelea kuipa timu muda zaidi ili kutathmini maendeleo yake baada ya wachezaji kupata nafasi ya kuzoeana, badala ya kufanya uamuzi wa haraka kwa kuzingatia matokeo ya sasa.
AS FAR pia ina sera ya kuepuka mabadiliko yasiyo ya lazima ya makocha, ikisisitiza kuwa kocha hapaswi kubeba lawama za matokeo mabaya bila kuwepo ushahidi wa wazi unaoonyesha kuwa maamuzi na kazi yake vimechangia mwenendo huo.
Hivyo, Goncalves anatarajiwa kuendelea na majukumu yake, huku mapumziko ya mechi za kimataifa yakitoa fursa kwa uongozi kufanya tathmini ya kina kuhusu kiwango cha timu na hatua zinazopaswa kuchukuliwa. Kwa sasa, AS FAR imeamua kuendelea na msimamo wa utulivu na uvumilivu, huku kocha huyo akipewa nafasi ya kubadili mwenendo wa kikosi chake.