Gwiji ampeleka Mbappe Arsenal
Muktasari:
- Petit, ambaye aliwahi kushinda Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa, amesema Mbappe anafaa sana katika mfumo wa kocha Mikel Arteta hasa upande wa kushoto wa ushambuliaji.
LONDON, ENGLAND: WAKATI mustakabali wa mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappe, ukiendelea kuwa gumzo licha ya kuwa mmoja wa nyota wakubwa wa klabu hiyo, kiungo wa zamani wa Monaco, Arsenal, Barcelona na Chelsea, Emmanuel Petit amesema Arsenal ndiyo timu inayomfaa zaidi Mbappe ikiwa ataamua kuondoka.
Petit, ambaye aliwahi kushinda Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa, amesema Mbappe anafaa sana katika mfumo wa kocha Mikel Arteta hasa upande wa kushoto wa ushambuliaji.
“Arsenal wangependa kuwa na Kylian Mbappe, na angefaa kabisa upande wa kushoto wa uwanja,” amesema Petit. Hata hivyo anaamini mchezaji huyo hataondoka Real Madrid kwa sasa kwa sababu anaamini kuondoka bila kushinda taji lolote itakuwa ni sawa na kufeli binafsi.
“Sababu pekee inayonifanya niamini Mbappe atasalia Real Madrid ni kwamba kuondoka bila kushinda taji kutafanya usajili wake uonekane kama umefeli. Ana lengo kubwa na atataka kubaki kuthibitisha uwezo wake,” amesema Petit.
Mbappe amecheza mechi 41 na kufunga mabao 41 katika mashindano yote msimu huu, lakini mafanikio yake binafsi hayajaisaidia Real Madrid kushinda mataji makubwa, ambapo ilipoteza ubingwa wa Ligi Kuu Hispania (La Liga) dhidi ya Barcelona baada ya kufungwa mabao 2-0 katika El Clasico ya Mei 10, huku pia ikitolewa Ligi ya Mabingwa Ulaya katika robo fainali.
Mbali na ukosefu wa mataji, pia kumekuwapo na sintofahamu ndani ya timu ikiwemo madai ya kutofautiana kati ya viungo nyota Federico Valverde na Aurelien Tchouameni pamoja na kutoridhishwa kwa baadhi ya mashabiki baada ya Mbappe kuonekana akiwa safarini na mwigizaji Ester Exposito wakati wa akiuguza majeraha yake. Kwa sasa kuna kampeni inayoendelea mtandaoni kukusanya saini za mashabiki wasiomtaka mchezaji huyo Real Madrid.
Hata hivyo, Petit amesema Arsenal inaweza kuwa sehemu bora zaidi kwa Mbappe hasa kama itashinda Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza. Kwa sasa hakuna mazungumzo rasmi kati ya Arsenal na Mbappe, lakini mjadala kuhusu mustakabali wake umeendelea kushika kasi.