Frimpong azigonganisha Liverpool, Manchester City
Muktasari:
- Tangu kuanza kwa msimu huu, Frimpong ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, amecheza mechi 38 za michuano yote na kutoa asisti 11.
LIVERPOOL na Manchester City zinapambana vitakuiwania saini ya beki wa kulia wa Bayer Leverkusen na timu ya taifa ya Uholanzi, Jeremie Frimpong, 24, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi na timu yake ipo tayari kusikiliza ofa inayoanzia Euro 40 milioni.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Frimpong ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, amecheza mechi 38 za michuano yote na kutoa asisti 11.
Mabosi wa Liverpool wanamwangalia fundi huyu kama mbadala wa Trent Alexander Arnold ambaye kuna uwezekano mkubwa akaondoka mwisho wa msimu huu baada ya mkataba wake kumalizika.
Kwa upande wa Man City, wanataka kumsajili beki huyu kama mbadala wa Kyler Walker ambaye ametimkia AC Milan katika dirisha lililopita.
Martin Zubimendi
ARSENAL ina matumaini makubwa ya kumsajili kiungo wa Real Sociedad na timu ya taifa ya Hispania, Martin Zubimendi, 26, ambaye aliamua kusalia Sociedad licha ya kupokea ofa ya kujiunga na Liverpool katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Zubimendi ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu huu amecheza mechi 32 za michuano yote.
Marc Guehi
CHELSEA imepanga kufanya kila linalowezekana kuhakikisha zinaipiku timu nyingine katika vita ya kuiwana saini ya beki wa Crystal Palace na England, Marc Guehi, 24, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Kwa mujibu wa ripoti kutoka tovuti ya The Mirror Palace inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 70 milioni ili kumuuza. Guehi alizivutia timu nyingi kutokana na kiwango bora alichoonyesha katika michuano ya Euro mwaka jana akiwa na timu ya taifa ya England.
Caoimhin Kelleher
GOLIKIPA wa Liverpool na Jamhuri ya Ireland, Caoimhin Kelleher, 26, ameendelea kuwa mmoja wa mastaa ambao Chelsea inataka kuwasajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kuboresha lango lao baada ya Kocha Enzo Maresca kutoridhishwa na viwango vya makipa wa sasa hususani Roberto Sanchez. Chelsea ipo tayari kulipa Pauni 40 milioni ili kumsajili Kelleher.
Lamine Yamal
WINGA wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Lamine Yamal, 27, amekanusha taarifa anafikiria kutua Paris St-Germain dirisha lijalo na kusisitiza mpango wake ni kuendelea kuitumikia Barca ambayo ipo moyoni mwake. Taarifa za Yamal kuhitajika na PSG zilianza kusambaa tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi na miamba hiyo ya Ufaransa inadaiwa iliweka mezani ofa inayofikia Euro 200 milioni.
Luis Diaz
MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Luis Diaz, 28, yupo tayari kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo kwa muda mrefu zaidi licha ya timu nyingine nyingi barani Ulaya kuonyesha nia ya kumsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi ikiwemo Barcelona. Mkataba wa Luis unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Msimu huu amefunga mabao 13 katika mechi 36 za michuano yote.
Franculino Dju
LEICESTER City na Crystal Palace zinamfuatilia kwa karibu mshambuliaji wa Midtjylland na Guinea-Bissau, Franculino Dju, 20, ili kuipata saini yake dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Dju ambaye amepitia katika akademi ya Benfica, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026 Msimu huu amecheza mechi 26 za michuano yote na kufunga mabao 10.
Jonathan Tah
BARCELONA inadaiwa kufikia makubaliano binafsi na beki wa Bayer Leverkusen, Jonathan Tah, 29, ambaye ameonyesha nia ya kujiunga nao licha ya kupokea ofa kibao kutoka kwa timu nyingine Ulaya ikiwemo Bayern Munich. Tah ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu aliweka wazi hatoongeza na ataondoka kwa ajili ya kutafuta changamoto mpya.