Ferdinand adai mchawi Man United ni presha
Muktasari:
- Mshambuliaji Marcus Rashford ni mchezaji aliyeondoka kwenye kikosi hicho dirisha lililopita kwa mkopo akienda kujiunga na Aston Villa. Na baada ya kucheza mechi yake ya kwanza Villa Park aliposti ujumbe kwenye Instagram akishukuru mashabiki kumpokea vema wakati timu yake mpya iliposhinda 2-1 dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye mchezo wa Kombe la FA.
MANCHESTER, ENGLAND: BEKI wa zamani, Rio Ferdinand amesema presha ya kuichezea Manchester United si mchezo ndiyo maana wachezaji wengi wanaondoka Old Trafford wanakwenda kung'ara huko kwingineko kwa sababu wanakuwa wameutua mzigo mkubwa vichwani mwao.
Mshambuliaji Marcus Rashford ni mchezaji aliyeondoka kwenye kikosi hicho dirisha lililopita kwa mkopo akienda kujiunga na Aston Villa. Na baada ya kucheza mechi yake ya kwanza Villa Park aliposti ujumbe kwenye Instagram akishukuru mashabiki kumpokea vema wakati timu yake mpya iliposhinda 2-1 dhidi ya Tottenham Hotspur kwenye mchezo wa Kombe la FA.
Winga Jadon Sancho, ambaye pia ameondoka Man United kwa mkopo huko Chelsea, alikomenti kwenye ujumbe huo wa Rashford alipoandika "uhuru". Staa huyo wa zamani wa Borussia Dortmund alicheza kwenye timu hiyo kwa mkopo msimu uliopita na sasa Chelsea kuna uwezekano wa mkubebwa jumla.
Wachezaji wengi wa zamani wa Man United wameonekana kucheza vizuri baada ya kuondoka kwenye timu hiyo, akiwamo Anthony Elanga, Scott McTominay na wa hivi karibuni Antony. Jambo hilo limemwibua Ferdinand na kufichua kile kinachowafanya wachezaji hao kung'ara wanapoondoka Old Trafford.
"Ona Antony, amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi baada ya kufunga na kuasisti katika mechi mbili," alisema Ferdinand, akizungumzia kiwango cha Mbrazili aliyekwenda kujiunga na Real Betis kwa mkopo dirisha lililopita.
"McTominay anacheza kama Jude Bellingham kwenye ubora wake kwa sasa. Yupo Elanga, ambaye amekuwa winga matata. Unaweza kuona wachezaji hao baada ya kuondoka Man United wamekuwa wachezaji wapya na kuonekana wapya kwa sababu wametua mzigo na kasheshe la presha ya kucheza Old Trafford, beji ina nguvu kubwa, wakiondoka wanapata nafuu na kuona utofauti wa kuwa kwenye timu nyingine. Hata kwa Rashford itakuwa hivyo hivyo. Kilichopo ni wameshindwa tu kutegua mtego wa kucheza kwenye eneo lenye presha kubwa kama la Old Trafford."
Rashford alianzia benchi kwenye mechi yake ya kwanza huko Villa Park na aliungana na mchezaji mwenzake waliyewasajiliwa wote Januari, Marco Asensio. Mastaa wengine wa Aston Villa iliyowasajili Januari, Andres Garcia na Donyell Malen wao walianzishwa, huku mabao ya Jacob Ramsey na Morgan Rogers yalisaidia kupata ushindi wa 2-1 na hivyo kutinga kwenye raundi ya tano ya Kombe la FA.
SIKIA HUU UTANI WA MASHABIKI
-Arsenal: Inaibua masupastaa
-Liverpool: Inatengeneza masupastaa
-Man City: Inaendeleza masupastaa
-Chelsea: Inanunua masupastaa
-Man United: Inaua masupastaa