Fainali Europa ni ya ufundi mwingi

Muktasari:
- Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya mbinu za kimchezo, wanachora mchoro, ambao utaweza kuipa moja ya timu zitakazochuana kwenye fainali hiyo, kubeba ubingwa.
BILBAO, HISPANIA: FAINALI ya Europa League itapigwa usiku wa Jumatano na miamba miwili ya Ligi Kuu England, Tottenham Hotspur na Manchester United itakutana yenyewe huko Estadio de San Mames, jijini Bilbao, Hispania. Itakuwaje?
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya mbinu za kimchezo, wanachora mchoro, ambao utaweza kuipa moja ya timu zitakazochuana kwenye fainali hiyo, kubeba ubingwa.
Unaambiwa hivi, nafasi atakayopangwa Bruno Fernandes dhidi ya kiungo sumbufu ya Tottenham ni kete muhimu kwenye kuisaidia Man United kushinda taji hilo la Europa League.
Uzuri wa fainali hiyo ni kila timu inajaribu kujitetea baada ya kuwa na msimu mbaya kwenye Ligi Kuu England.
Zama za Kocha Ruben Amorim kwenye kikosi cha Man United zimekuwa za ovyo na wachezaji wa timu hiyo bado hawaonekani kuuweza mtindo wake wa uchezaji wa 3-4-3.
Lakini, kama Man United itaweka mbinu zake sawa, ina uwezo wa kuisambaratisha Spurs, ambayo itacheza bila ya huduma ya wakali James Maddison, Dejan Kulusevski na Lucas Bergvall kwenye eneo la kiungo.
FERNANDES ACHEZE WAPI?
Amorim ana machaguo mengi - ama amtumie nahodha wake huyo kama mmoja wa Namba 10 au ampange chini kwenye safu ya viungo wawili wa kati. Man United inapaswa kuwaamini Casemiro na Manuel Ugarte kuanza nao kwenye sehemu ya kiungo ili kumfanya Fernandes kuwa huru na kufanya mambo yake ya kupandisha mipira mbele.
Fernandes anapocheza kama mmoja wa Namba 10, amekuwa na uwezo wa kupita nyuma ya viungo wa upinzani na kuitanua safu ya mabeki. Lakini, mtindo huo unaweza kumpa wakati mgumu Fernandes, hasa anapocheza dhidi ya Micky van de Ven, inaweza kuleta shida.
Amorim anachopaswa kufanya ni kuhakikisha anamfanya Fernandes kuwa huru uwajani, asicheze eneo moja ili kuipa kizunguzungu Spurs.
Kocha wa Spurs, Ange Postecoglou atataka timu yake kuikabia juu Man United, kama itaamua kukaa na mpira kwenye eneo lao. Kumtumia Fernandes kwenye nafasi yake ya asili, Namba 10 wa kati, kutailazimisha Spurs kumshusha kiungo mmoja aje kupambana na Mreno huyo, la watakuwa kwenye hatari ya kukabilisha wachezaji watatu kwa wawili. Bruno akicheza kwenye eneo hilo, kutaifanya Spurs kuhakikisha inakuwa na wachezaji watatu wa kukabiliana naye.
Bila shaka Spurs italazimika kupitia pembeni, upande wa kushoto wa Destiny Udogie. Fernandes kitu ambacho atapaswa kufanya asikimbize mpira kwenye kumkaba Udogie, badala yake atumie pengo atakalokuwa ameliacha mchezaji huyo kuiadhibu Spurs.
Spurs inapenda kujaa upande wa kushoto, hivyo kuhamisha mpira kwa haraka kwenda upande mwingine unaweza kuiweka Spurs kwenye uwazi mkubwa wa kushambuliwa kwa urahisi.
FERNANDES ASICHEZE CHINI
Kama nahodha huyo wa Man United atacheza chini kama moja wa viungo wawili, hilo litawafanya wabanwe na kushambuliwa na Spurs kitu kitakachowapa ugumu wa kwenda mbele kujibu mashambulizi kwa urahisi. Man United itapata shida kukabiliana na Spurs yenye kawaida ya kukabia juu kama Fernandes hatatumika kwenye eneo ambalo linamfanya awe anatumia akili yake kwa usahihi anapokuwa karibu na goli la wapinzani. Uzuri wa Fernandes anaposogelea goli la wapinzani amekuwa na ujuzi mkubwa wa kutengeneza nafasi, kitu ambacho Spurs haitapenda kumpa uhuru huo Fernandes kuzurura na mipira nje ya boksi lao.
Kufanya mashambulizi ya kushtukiza si kitu kitakachowafanya Man United kuwa na wakati mzuri kutokana na Rasmus Hojlund kutokuwa na uwezo wa kutulia na mipira kwenye miguu yake, huku Alejandro Garnacho kutokuwa na hesabu nzuri kwenye kasi yake, kunaweza kumfanya Van de Ven kuwa na usiku nzuri kabisa kwenye beki ya Spurs.
JE, AMAD ACHEZE WING-BACK?
Amad Diallo anaweza kuwa wing-back wa muda mrefu wa kocha Amorim, lakini si katika mchezo huo wa fainali. Hiyo ni kwa sababu, mabeki wa pembeni wa Spurs wataingia ndani kuwaruhusu mabeki wao wa kati kutanua uwanja na kupiga pasi ndefu kwa winga wao. Kutokana na hilo, Amad atakuwa kwenye hatari ya kulazimishwa kurudi chini na kuna nyakati atajikuta kwenye shughuli ya kukabana ana kwa ana na washambuliaji wa Spurs, huku yeye ikifahamika wazi si hodari kwenye kukaba. Amad akicheza mbele, jambo hilo litawafanya mabeki wa Spurs kuwa na wasiwasi wa kwenda mbele kwa kuhofia kuumizwa na staa huyo. Kwa jambo hilo, itakuwa salama zaidi kwa kocha Amorim kuwatumia Noussair Mazraoui na Patrick Dorgu kwenye wing-back. Na kwamba Amad aanzie benchi, aingie baadaye kuongeza nguvu kuja kuisumbua beki ya Spurs kwa wakati ambao itakuwa imechoka.
JE, MAN UNITED ITAIKABIA JUU SPURS?
Si kitu kinachofanywa sana na kocha Postecoglou, lakini msimu huu hasa kwenye michuano ya Ulaya amekuwa na mtindo tofauti wa kucheza, akiiweka chini timu yake na kufanya mashambulizi ya kushtukiza. Lakini, kwenye fainali hiyo akijaribu kucheza kwa mtindo huo wa kuwasubiri wapinzani chini, timu yake inaweza kuwa kwenye wakati mgumu na Man United ikawakabia kwa juu na kutumia nguvu yao kwenye upande wa kushoto kuwaadhibu Spurs.
Man United inapenda kusambaza mpira kwenye muundo wa W, ambapo viungo wake wawili na mabeki wa kati wanapanda juu kutoa wakati mgumu kwa wapinzani, mtindo ambao waliotumia kwenye mechi za karibuni za michuano ya Europa League na kufanikiwa kufika fainali. Kwenye mtindo huo, Fernandes atakuwa huru kwenye mpira, kitu ambacho ni hatari kwa wapinzani.
SPURS ITASHINDA VIPI?
Kukosekana kwa Maddison, Kulusevski na Bergvall, inaonyesha Spurs itacheza kwa kujilinda sana na kutumia nguvu kwenye sehemu ya kiungo. Badala ya kutumia fomesheni yao pendwa ya 4-2-3-1, kocha Postecoglou anaweza kulazimika kutumia 4-3-3. Atahitaji kuwa na mtu wa ziada kwenye sehemu ya kiungo ili kusaidia kuwapa wakati mgumu viungo wa Man United na kumnyima Fernandes uhuru wa kuwa na mpira bila ya purukushani yoyote. Spurs itawatumia Udogie na Porro kwenye kushambulia kuwabana wing-back wa Man United ili kulazimika kuzuia na wachezaji watano badala ya watatu. Jambo hilo litaifanya Man United kuacha maeneo mengine kuwa wazi, ambayo Spurs wanaweza kuyatumia na kuwaadhibu wapinzani.
Lakini, kukosekana kwa Maddison au Kulusevski watu wenye uwezo wa kutumia nafasi hizo kwa pasi zao matata za mwisho, linaweza kuwa pigo kubwa kwa Spurs. Lakini, Spurs inaweza kuipa wakati mgumu Man United kwa kuikabia juu, kuwalazimisha wapinzani wao wafanye mashambulizi ya kushtukiza ambao hayatakuwa na tishio lolote kutokana na straika wao Hojlund kuonekana kutokuwa na uwezo wa kuwazidi maarifa Van de Ven na Cristian Romero.