Eh! Vita mpya yaibuka sokoni, Napoli yajitosa dili la Gyokeres

Muktasari:
- Mabosi wa Napoli wanataka kutumia kiasi cha pesa ambacho watakipata kupitia mauzo ya Victor Osimhen kufanya usajili wakiamini atakuwa ni mbadala wake sahihi.
NAPOLI ni kati ya timu zilizoingia katika vita ya kuiwania saini ya straika wa Sporting Lisbon na timu ya taifa ya Sweden, Viktor Gyokeres ambaye anawindwa na vigogo kadhaa kutoka England ambao ni pamoja na Arsenal, Manchester United na Chelsea.
Mabosi wa Napoli wanataka kutumia kiasi cha pesa ambacho watakipata kupitia mauzo ya Victor Osimhen kufanya usajili wakiamini atakuwa ni mbadala wake sahihi.
Hata hivyo, haionekani kama mabingwa hawa wa Serie A wanaweza kushinda vita hii kutokana na upinzani mkali uliopo kutoka kwa wapinzani wao.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, lakini Sporting iko tayari kumuuza kwa ada ya uhamisho iliyo chini ya Pauni 60 milioni.
Msimu huu amecheza mechi 52 za michuano yote na kufunga mabao 54.
Pedro Goncalves
MANCHESTER United wanataka kumsajili kiungo wa kati wa Sporting Lisbona na timu ya taifa ya Ureno, Pedro Goncalves, mwenye umri wa miaka 26, kama mbadala wa kiungo mwenza wa Ureno, Bruno Fernandes, 30, iwapo ataondoka kwenda Saudi Arabia katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Pedro ni miongoni mwa wachezaji walioonyesha kiwango bora katika kikosi cha Lisbon hususani msimu uliopita.
Eberechi Eze
BAYERN Munich inavutiwa kumsajili kiungo wa kati wa kimataifa wa England na Crystal Palace, Eberechi Eze, mwenye umri wa miaka 26, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mabosi wa Munich wamepatwa na tamaa ya kumsajili Eze baada ya kuona staa waliyemsajili kutoka Palace, Michael Olise amekuwa katika kiwango bora. Hata hivyo, mabosi wa Palace wanataka asaini mkataba wa kuendelea kusalia kwenye kikosi chao.
Cody Gakpo
WINGA wa Liverpool na timu ya taifa ya Uholanzi, Cody Gakpo, mwenye umri wa miaka 26, na winga wa Japan wa Brighton, Kaoru Mitoma, 28, pia wapo kwenye orodha ya wachezaji wanaowindwa na Bayern Munich kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Gakpo na Mitoma ni miongoni mwa washambuliaji walioonyesha kiwango bora katika EPL kwa msimu uliomalizika.
Rodrygo
MSHAMBULIAJI wa Real Madrid na Brazil, Rodrygo, mwenye miaka 24, anadaiwa kuiambia timu hiyo kwamba anahitaji kuendelea kusalia kwenye timu hiyo licha ya vigogo kadhaa wa England kuanza kumnyemelea ili kuipata saini yake katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Rodrygo alihusishwa sana kuwa katika mpango wa kuondoka wakati msimu unaelekea kumalizika.
Rayan Cherki
MANCHESTER City itawasilisha ofa ya awali wiki hii kwa ajili ya kumsajili kiungo wa kati wa Olympique Lyon na timu ya taifa ya Ufaransa chini ya miaka 21, Rayan Cherki, mwenye miaka 21, katika dirisha lijalo.
Cherki ambaye mkataba wake wa sasa na Lyon unatarajiwa kumalizika mwaka 2026, msimu huu amecheza mechi 44 za michuano yote na kufunga mabao 12.
Rodri
KIUNGO wa kati wa Hispania, Rodri, atapewa mkataba mpya na Manchester City hivi karibuni ambao utakuwa na ongezeko kubwa la mshahara ikiwa ni sehemu ya kutambua ukubwa wake baada ya kushinda tuzo ilioyopita ya Ballon Do’r. Mkataba wa sasa wa Rodri unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Anatajwa kama kukosekana kwake msimu uliopita, kuliiathiri sana Man City.
Marcus Rashford
BARCELONA imesitisha mpango wao wa kutaka kumsajili mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford, mwenye miaka 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi na itamrudia tu endapo dili la kumsajili winga wa Liverpool na timu ya taifa ya Colombia, Luis Diaz mwenye miaka 28, halitatimia.