Dogo Bayern kuandika historia Ulaya
Muktasari:
- Bayern inakabiliwa na makipa wote wakubwa kuwa majeruhi na Prescott (16) ndiye suluhisho la mwisho katika mchezo huo wa mkondo wa pili wa Ligi ya mabingwa Ulaya na sheria ya nchi hiyo inaruhusu tofauti na ya England.
MUNICH, UJERUMANI: LEONARD Prescott anatarajiwa kuandika historia atakaposimama langoni leo, Bayern Munich itakapoikaribisha Atalanta kwenye Uwanja wa Allianz Arena, Ujerumani kuanzia saa 5:00 usiku.
Bayern inakabiliwa na makipa wote wakubwa kuwa majeruhi na Prescott (16) ndiye suluhisho la mwisho katika mchezo huo wa mkondo wa pili wa Ligi ya mabingwa Ulaya na sheria ya nchi hiyo inaruhusu tofauti na ya England.
Sheria ya Ligi Kuu England inawalinda makiba wenye umri mdogo kucheza katika mechi za timu kubwa ili kuwaepusha mikikimikiki ya mechi hasa mashuti makali ya wapinzani na namna ya kuwakabili washambuliaji wakubwa.
Kocha Vincent Kompany amepoteza makipa wake wanne wa kikosi cha wakubwa kutokana na majeraha na Sven Ulreich ndiye wa mwisho kuumia katika mechi ya Bundesliga dhidi ya Bayer Leverkusen, Jumamosi iliyopita katika sare ya bao 1-1.
Ulreich aliyeanza katika mchezo huo, alipata jeraha la misuli ya paja na anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa muda na anaungana na kipa namba moja, Manuel Neuer, 39, ambaye naye ana majeraha ya mguu na anatarajiwa kurudi baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
Kipa Jonas Urbig alipata mtikisiko wa ubongo (concussion) katika mechi ya kwanza ya hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa na Bayern ilishinda 6-1 ugenini dhidi ya Atalanta.
Kutokana na jeraha hilo la Ulreich, huenda leo langoni akasimama Prescott mzaliwa wa New York, Marekani ambaye alikuwa benchi katika mechi mbili zilizopita za Bayern, huku kipa mwingine Leon Klanac naye akiwa nje kwa muda mrefu.
Katika ligi za England, timu huruhusiwa kusajili kipa wa dharura kwa mkopo iwapo wote wameumia, lakini sheria hiyo haipo katika Ligi ya Mabingwa.
Mtaalamu wa soka la Ulaya, Andy Brassell, alithibitisha hilo akisema Bayern hawana chaguo jingine la kipa kwa sasa.
“Kama kweli ni tatizo wakati huu wakiwa wanaongoza 6-1 kutoka mchezo wa kwanza, ni wazi hawana makipa waliobaki."
Prescott ambaye alichagua kuichezea Ujerumani katika ngazi za vijana kuanzia U15, U16 na U17, iwapo ataanza, atakuwa kipa mdogo zaidi katika historia ya Bayern Munich na mdogo zaidi katika historia ya Ligi ya Mabingwa.
Akiwa na miaka 16 na siku 176, atakuwa mchezaji wa nane kwa udogo kuwahi kucheza mashindano hayo, huku rekodi ya juu ikishikiliwa na mchezaji wa Arsenal.
Kipa huyo mwenye urefu wa mita 1.96 amekuwa akicheza zaidi katika kikosi cha vijana cha Bayern cha U19 msimu huu tangu ajiunge kutoka Union Berlin 2023.
Hadi sasa, amecheza mechi 16 katika kikosi cha U19 na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa Vijana, akifanikiwa kuwa na clean sheet moja na kuruhusu mabao 30.
MADOGO WALIOKIPIGA ULAYA MAPEMA
Max Dowman (miaka 15 na siku 308)
Youssoufa Moukoko (miaka 16 na siku 18)
Lamine Yamal (miaka 16 na siku 68)
Celestine Babayaro (miaka 16 na siku 86)
Rayan Cherki (miaka 16 na siku 102)
Marli Salmon (miaka 16 na siku 103)
Alen Halilovic (miaka 16 na siku 128)
Youri Tielemans (miaka 16 na siku 148)
Francesco Camarda (miaka 16 na siku 226)
Warren Zaire-Emery (miaka 16 na siku 228)
Charalampos Mavrias(miaka 16 na siku 241)