Delap azipagawisha Chelsea na Manchester United
Muktasari:
- Man United inamwangalia kama mbadala sahihi wa Marcus Rashford aliyetolewa kwa mkopo kwenda Aston Villa na huenda akauzwa mwisho wa msimu.
MANCHESTER United na Chelsea zipo katika vita ya kuwania huduma ya straika wa Ipswich Town na England, Liam Delap, 21, ambaye ni miongoni mwa wafungaji waliofanya vizuri tangu kuanza kwa msimu huu ambapo amefunga mabao tisa katika mechi 25 za michuano yote.
Man United inamwangalia kama mbadala sahihi wa Marcus Rashford aliyetolewa kwa mkopo kwenda Aston Villa na huenda akauzwa mwisho wa msimu.
Man U na Chelsea zimekuwa na uhitaji wa mshambuliaji tangu dirisha la majira kiangazi mwaka jana, lakini zilishindwa kufanikisha saini za mastaa ziliowataka.
Delap ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2029, anaweza kuuzwa mwisho wa msimu lakini ada yake ya uhamisho inaweza kuwa Pauni 60 milioni. Awali Ipswich ilimchukua kwa mkopo msimu mmoja kutoka kikosi cha pili cha Man City dirisha lililopita, lakini ilitumia kipengele cha kumnunua kilichokuwepo kwa kulipa Euro 17 milioni.
Alejandro Balde
MANCHESTER United ipo tayari kuwasilisha ofa ya Pauni 33.3 milioni kwenda Barcelona katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kuipata saini ya beki wa kushoto wa timu hiyo na Hispania, Alejandro Balde. Mabosi wa Man United wanaamini Barca itakuwa tayari kumuuza beki huyo ikiwa ni katika harakati za kutaka kupunguza baadhi ya mastaa ilionao ili kuweza kusajili wengine wapya.
Johan Bakayoko
NEWCASTLE United inajindaa kuwasilisha ofa ya Euro 40 milioni kwenda PSV Eindhoven ili kuipata huduma ya mshambuliaji wa timu hiyo na Ubelgiji, Johan Bakayoko, 21, katika dirisha lijalo. Bakayoko alikuwa akihusishwa na timu nyingi kubwa Ulaya tangu dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, lakini ilishindikana baada ya PSV kugoma kumuuza kwa kuwa haikupata ofa iliyoitaka.
Antonio Cordero
NEWCASTLE United inataka kuzipiku Barcelona na Real Madrid kuwania saini ya winga wa Malaga, Mhispania Antonio Cordero ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Malaga imekuwa ikijaribu kumshawishi asaini mkataba mpya ili asiondoke bure, lakini Cordero, 18, amekataa na kusisitiza kwamba anataka kuondoka.
Moise Kean
FIORENTINA inajipanga kumsainisha mkataba mpya straika Moise Kean ambaye hivi karibuni ameingia kwenye rada za Tottenham Hotspur na Arsenal zinazompigia hesabu kwa ajili ya kumsajili katika dirisha lijalo. Kwa mujibu wa taarifa, vigogo wa Fiorentina wanataka kumsainisha mkataba mpya u ili kubadilisha kipengele kinachotaja pesa inayotakiwa kutolewa ikiwa timu yoyote inahitaji saini yake.
Dario Essugo
CHELSEA imetuma maskauti wake kwenda Hispania kwa ajili ya kumtazama kiungo wa Sporting Lisbon na Ureno, Dario Essugo ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Las Palmas inayoshiriki La Liga. Kwa mujibu wa taarifa ya awali kutoka kwa maskauti hao, staa huyo mwenye umri wa miaka 19 anafaa kusajiliwa. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2027.
Dean Huijsen
BEKI wa Bournemouth na Uholanzi, Dean Huijsen ni miongoni mwa mastaa waliopendekezwa na kocha wa Chelsea, Enzo Maresca akitaka asajiliwe katika dirisha la majira ya kiangazi mwakani. Beki huyo amekuwa mhimili muhimu katika safu ya ulinzi ya Bournemouth kiasi cha kuzivutia timu nyingi ikiwamo Liverpool.
Joan Garcia
ARSENAL ina matumaini makubwa kwamba hakuna kitakachoharibika na watafanikisha mpango wa kumsajili kipa wa Espanyol na Hispania, Joan Garcia, 23, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.Garcia anahitajiwa na Arsenal kwa ajili ya kwenda kumpa changamoto David Raya ambaye hivi karibuni amekuwa na makosa yanayolifikirisha benchi lake la ufundi.