De Bruyne, Jonathan David wanukia Napoli

Muktasari:
- Mikataba ya mastaa hawa inatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na tayari wameshafikia makubaliano ya kuachana na timu wanazozitumikia kwa sasa.
MABINGWA wa Italia, Napoli wanatarajiwa kukamilisha usajili wa wachezaji wawili kwa uhamisho wa bure, ambao ni kiungo wa kati kutoka Ubelgiji, Kevin De Bruyne, mwenye umri wa miaka 33 na mshambuliaji wa Lille na timu ya taifa ya Canada, Jonathan David.
Mikataba ya mastaa hawa inatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na tayari wameshafikia makubaliano ya kuachana na timu wanazozitumikia kwa sasa.
Ripoti zinasema kuwa, Napoli imetenga mshahara unaofikia Pauni 100,000 kwa wiki, lakini atakuwa na bonasi ambazo kwa ujumla zinaweza kumwezesha kupata hadi Pauni 300,000 kwa wiki.
Fundi huyu anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Pauni 21 milioni.
Marc Guehi
KLABU ya Newcastle United iko tayari kuanza mchakato wa kufanya usajili wa kikosi hicho kipindi hiki kufunguliwa dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa kutuma ofa kwenda Crystal Palace kwa ajili ya kuipata saini ya beki kisiki wa timu hiyo na England, Marc Guehi (24) pamoja na mshambuliaji wa Brentford na timu ya taifa ya Cameroon, Bryan Mbeumo mwenye umri wa miaka 25.
Jordan Henderson
KIUNGO wa kimataifa wa England, Jordan Henderson (34), huenda akaachana na Ajax ya Uholanzi na kurudi England kujiunga na Sunderland katika dirisha lijalo.
Sunderland iliyopanda daraja msimu huu, imevutiwa sana na Henderson na wanaamini wakimpata ataongeza kitu katika chumba cha kubadilishia nguo kutokana na uzoefu alionao.
Pedro Goncalves
MANCHESTER United inavutiwa na kiungo wa Sporting na Ureno, Pedro Goncalves (26) na inatarajiwa kuanza mazungumzo na wawakilishi wake hivi karibuni.
Pedro ambaye msimu huu amechukua ubingwa akiwa na Lisbon, amekuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza cha wababe hao kwa muda mrefu.
Jakub Kiwior
BEKI wa Arsenal na timu ya taifa ya Poland, Jakub Kiwior, mwenye umri wa miaka 25, anawindwa tena na Napoli kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Licha ya kuhitaji saini ya beki huyo tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Napoli inahitaji Arsenal ikubali kupunguza bei ya nyota huyu. Kwa sasa Arsenal inahitaji Pauni 30 milioni ili kumuuza.
Ferran Torres
ASTON Villa imeanza mazungumzo kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Ferran Torres, mwenye umri wa miaka 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Taarifa zinaeleza, Villa ipo tayari kutoa kiasi kisichopungua Pauni 42 milioni. Mkataba alionao sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027..
David Hancko
AC Milan imefikia hatua nzuri katika mpango wa kumsajili beki wa kati wa Feyenoord, David Hancko kuelekea dirisha lijalo, lakini inakumbana na ushindani mkubwa kutoka kwa Bayer Leverkusen na Juventus ambazo zimeonyesha nia ya kumsajili beki huyo wa kimataifa wa Slovakia mwenye umri wa miaka 27. Mkataba alionao kwa sasa unaisha mwaka 2028.
Mark Flekken
BAADA ya kutambulishwa hivi karibuni, kocha mpya wa Bayer Leverkusen, Erik ten Hag ameripotiwa kuwasilisha jina la kipa wa Brentford, Mark Flekken (31), akihitaji asajiliwe katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kipa huyu wa kimataifa wa Uholanzi, mkataba alionao na Brentford unatarajiwa kumalizika Juni 30,2027.