Darwin Nunez anukia kutua Saudia, Al Hilal yatajwa

Muktasari:
- Hata hivyo, staa huyu hatoweza kujiunga kwa saa bali atasubiri hadi michuano ya Kombe la Dunia la klabu litakapomalizika.
MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Darwin Nunez huenda akaondoka Liverpool dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya Al-Hilal ya Saudi Arabia kuanza mawasiliano na wawakilishi wake ya kumsajili.
Hata hivyo, staa huyu hatoweza kujiunga kwa saa bali atasubiri hadi michuano ya Kombe la Dunia la klabu litakapomalizika.
Ripoti kutoka tovuti ya talksports, Al-Hilal iliwasiliana na Liverpool Jumatatu ya wiki hii kuulizia uwezekano wa kuipata saini ya Nunez mwenye umri wa miaka 25.
Kwa sasa Liverpool ambayo ilikataa ofa ya Pauni 59 milioni Januari mwaka huu iliyowasilishwa na Al Nassr ya Saudi Arabia, iko tayari kumuuza mchezaji huyu lakini kwa kiasi kisichopungua Pauni 59 milioni.
Jack Grealish
EVERTON na Newcastle zinaongoza mbio za kumsajili mshambuliaji wa Manchester City na England, Jack Grealish, 29, kutoka Manchester City dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Grealish amepewa mkono wa kwa heri na Man City baada ya msimu uliopita kumalizika, huku pia jina lake likiachwa kati ya nyota watakaosafiri na timu kwenda Marekani. Licha ya timu za England huduma yake pia inahitajika na timu za Ujerumani ikiwemo Bayer Leverkusen.
Leroy Sane
WINGA wa kimataifa wa Ujerumani, Leroy Sane, 29, amekataa ofa kutoka Al-Hilal ya Saudi Arabia iliyomhitaji kumsajili kabla ya Juni 10 na badala yake anadaiwa kukubali ofa ya kujiunga na Galatasaray. Awali fundi huyu alikuwa katika mazungumzo ya kusaini mkataba mpya na Bayern Munich lakini ripoti zinadai yamefeli, hivyo ataondoka na huko Uturuki mashabiki wameonyeshwa kuvutiwa naye na kumkaribisha.
Vladimir Coufal
EVERTON, Wolves na Fulham zipo katika mazungumzo na beki wa kulia kutoka Jamhuri ya Czech, Vladimir Coufal, mwenye umri wa miaka 32, ambaye msimu uliopita alicheza mechi 25, za michuano yote. Beki huyu kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na West Ham msimu uliopita. Benchi la ufundi la ufundi la West Ham linadaiwa kusitisha mazungumzo ya kumsainisha mkataba mpya kwa sababu ya umri wake.
Nico Williams
ATHLETIC Bilbao ina matumaini ya kufikia makubaliano ya kumwongeza mshahara na mkataba mpya winga wao wa kimataifa wa Hispania mwenye umri wa miaka 22, Nico Williams, ambaye anahitajika na Bayern Munich, Arsenal na Chelsea. Nico ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Bilbao na mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Junior Firpo
REAL Betis imewasilisha ofa ya mkataba wa miaka mitatu kwa beki wa kushoto wa Jamhuri ya Dominika, Junior Firpo, ambaye mkataba wake na Leeds unakaribia kumalizika. Licha ya kuwasilisha ofa hiyo, mchezaji mwenyewe inadaiwa kutokuwa na mpango wa kujiunga nao badala yake kipaumbele chake kikubwa ni kuendelea kubakia Leeds au kujiunga na Olympique Lyon ambayo pia inahitaji huduma yake.
Djordje Petrovic
KIPA wa Chelsea na timu ya taifa ya Serbia, Djordje Petrovic ambaye ameachwa England wakati kikosi hicho kikiendaa Marekani kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia la klabu, yupo katika mazungumzo na Leeds United inayopambana kumsajili dirisha hili. Kipa huyu ameomba kubaki ili kupambania mchakato wa kutafuta timu mpya itakayompa nafasi ya kucheza.
Rodrygo
MSHAMBULIAJI wa Brazil, Rodrygo, 24, anataka kubaki Real Madrid na kupambania nafasi katika kikosi hicho chini ya kocha mpya, Xabi Alonso kuelekea msimu ujao. Rodrygo ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, awali alikuwa akihusishwa kuondoka na timu kibao kutoka England zilishaanza kuinyemelea huduma yake.