Danny Murphy: Arne Slot amejiweka kwenye hatari ya kufukuzwa
Muktasari:
- Liverpool ikicheza kwenye dimba la Anfield, ilikubali kichapo cha mabao 4-1, kilichoongeza machungu kwa mabingwa hao wa England, ambao wamekuwa na matokeo mabaya kwa siku za karibuni.
Aliyekuwa kiungo wa Liverpool, Danny Murphy, ameibuka na kutoa maoni yake kuhusu mustakabali wa kocha wa timu hiyo, Arne Slot, kufuatia kiwango cha timu hiyo kilichopelekea kupoteza mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSV, jana Jumatano, Novemba 26, 2025.
Liverpool ikicheza kwenye dimba la Anfield, ilikubali kichapo cha mabao 4-1, kilichoongeza machungu kwa mabingwa hao wa England, ambao wamekuwa na matokeo mabaya kwa siku za karibuni.
Murphy, ambaye aliichezea Liverpool karibu mechi 250, anaamini Slot huenda akajikuta katika shinikizo kubwa iwapo mwenendo huu utaendelea katika mechi zinazofuata.
“Kocha yeyote anayepitia kipindi ambacho anapoteza mara kwa mara, bila shaka anaweka kazi yake hatarini,” amesema kupitia talkSPORT.
“Kwa sasa, kiwango cha Liverpool kwenye ligi kinafanana na cha timu inayopambana kuepuka kushuka daraja. Ni Wolves pekee waliokusanya pointi chache katika mechi sita zilizopita. Kwa hiyo wakipoteza mechi mbili zijazo dhidi ya West Ham na Sunderland, bila shaka Slot atakuwa kwenye hatari.
“Natumai hatutafikia hatua hiyo. Ninampenda Slot hasa baada ya kukutana naye, ni mtu mwerevu, mpole na mwenye mvuto. Lakini haijalishi ulifanya nini awali au kama unapendwa. Hayo hayamaanishi chochote unapopoteza mechi mara kwa mara ukiwa na Liverpool. Hivyo, ana wiki muhimu sana mbele yake,” amesema.
Kutokana na matokeo hayo mabaya msimu huu, Liverpool sasa imeshuka hadi nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya EPL. Katika Ligi ya Mabingwa, kipigo cha jana Jumatano kimewaondoa kwenye nafasi za kufuzu moja kwa moja, na kwa sasa wako nafasi ya 13.
Mechi inayofuata ya Ligi ya Mabingwa, Liverpool itakipiga mapema mwezi Desemba 2025 dhidi ya Inter Milan ugenini, kisha itasafiri kwenda Marseille, Januari 2026. Majogoo hao wa jiji watahitimisha hatua ya makundi kwa kuivaa Qarabag, huku ikihitaji kuepuka kupoteza pointi zaidi ili kusonga mbele kwenda hatua ya mtoano moja kwa moja.