Cunha ni suala la muda Man United

Muktasari:
- Wolves imewapa Man United ruhusa ya kukamilisha dili hilo, ambalo linatarajiwa kuwa mkataba wa miaka mitano kwa Cunha, ukiwa na chaguo la kuongeza mwaka mmoja zaidi.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United wamekubaliana na Wolves juu ya kulipa Pauni 62.5 milioni kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa kumsajili staa wao Matheus Cunha katika dirisha lijalo.
Wolves imewapa Man United ruhusa ya kukamilisha dili hilo, ambalo linatarajiwa kuwa mkataba wa miaka mitano kwa Cunha, ukiwa na chaguo la kuongeza mwaka mmoja zaidi.
Wolves walikataa ofa za awali za Man United ambazo zilikuwa zinaonyesha kwamba kiasi hicho cha pesa kitalipwa ndani ya miaka minne au mitano kwa sababu wao walihitaji malipo yafanywe kwa awamu tatu ndani ya miaka miwili ambapo kiasi cha kwanza kitakachotakiwa kuwekwa kwenye akaunti ni Pauni 20.85 milioni.
Baada ya majadiliano ya muda mrefu, Man United wamekubali kulipa kiasi hicho kwa miaka miwili, hivyo sasa wanachokifanya ni kuzungumza na nyota huyo wa kimataifa wa Brazil ili kujadili maslahi binafsi.
Baadhi ya ripoti zinaeleza kwamba tayari wameshakubaliana maslahi binafsi na wawakilishi wa fundi huyo ambapo atasaini mkataba wa miaka mitano na nyongeza ya mwaka mmoja ikiwa wataridhishwa na kiwango chake.
Cunha anatarajiwa kusafiri kwenda Manchester kabla ya mwisho wa wiki kwa ajili ya vipimo vya afya, na atapewa jezi namba 10 iliyokuwa ikivaliwa na Marcus Rashford.
Licha ya kufikia makubaliano ya kumsajili Cunha ripoti zinaeleza, kocha wa mashetani hao wekundu Ruben Amorim bado anahitaji kuboresha zaidi eneo la ushambuliaji na mmoja kati ya mastaa ambao anawajitaji kwa sasa ni Bryan Mbeumo wa Brentford.
Hata hivyo, ili kufanikisha hilo kwanza watatakiwa kuuza baadhi ya wachezaji ambao ni pamoja na Alejandro Garnacho ambaye anauzwa kwa kati ya Pauni 60 hadi 70 ilioni, pia kuna uwezekano wa kupata Pauni 100 milioni kwa ajili ya kumuuza Bruno Fernandes.
Man United pia wanapanga kuwauza Rashford, Jadon Sancho, Antony, na Tyrell Malacia wakati Christian Eriksen, Victor Lindelof, na Jonny Evans wakitarajiwa kuondoka kama wachezaji huru mwisho wa msimu wa mwezi ujao.
Mail Sport ilifichua mwezi uliopita kwamba United walikuwa karibu na makubaliano na Wolves kuhusu usajili wa Cunha.
Cunha na Amorim walionekana wakizungumza April mwaka huu baada ya kipigo cha pili cha Man United dhidi ya Wolves msimu huu.
Msimu huu Cunha alifunga mabao 15 na kutoa asisti sita katika mechi 33 za Ligi Kuu England.
Kwa ulinganisho, Cunha amefunga mabao mengi zaidi kuliko mchezaji yoyote wa Man United kwa msimu ambapo mastaa Bruno Fernandes na Amad Diallo wanaoongoza katika kikosi hicho kila mmoja ana mabao nane tu.
Wolves walionekana kuwa njiani kumaliza juu ya United kwenye msimamo baada ya kuwafunga nyumbani na ugenini, lakini walipitwa siku ya mwisho ya msimu.
Ushindi wa mabao 2-0 wa Man United dhidi ya Aston Villa Jumapili, pamoja na sare ya Wolves ya 1-1 dhidi ya Brentford, uliihakikisha Man United kumaliza juu ya Wolves kwa tofauti ya mabao.
Hata hivyo, nafasi ya 15 bado ilikuwa ni nafasi ya chini zaidi kwa mashetani hao wekundu kwenye ligi tangu waliposhushwa daraja mwaka 1974.