Casemiro ampendekeza Bruno Man United
Muktasari:
- Kiungo huyo wa Brazil tayari alithibitisha mapema mwaka huu kuwa ataondoka Old Trafford baada ya mkataba wake kumalizika. Kulikuwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi, lakini hakitatumika.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO Casemiro amemtaja staa wa Newcastle United, Bruno Guimarães, kama chaguo bora la usajili ambao mabosi wa Manchester United wanapaswa kuufanya dirisha lijalo la usajili wakati yeye atakapoondoka Old Trafford.
Kiungo huyo wa Brazil tayari alithibitisha mapema mwaka huu kuwa ataondoka Old Trafford baada ya mkataba wake kumalizika. Kulikuwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi, lakini hakitatumika.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Hispania AS, Guimarães yuko juu kabisa kwenye orodha ya wachezaji wanaotazamwa na Man United na inapendekezwa kuwa Casemiro mwenyewe amempendekeza kwa mabosi anaswe kuja kuchukua mikoba yake.
Na Man United wanaonekana kumwona kama mchezaji muhimu kwa mustakabali wa timu. Mbali na Guimarães, nyota mwingine wa Newcastle United, Sandro Tonali, pia anaripotiwa kuzingatiwa, huku Man United wakidaiwa kuwa mbele ya Juventus katika mbio za kumsajili kutokana na changamoto za kifedha zinazolikabili klabu hiyo ya Italia.
Hata hivyo, Newcastle hawatakuwa tayari kuwaachia kirahisi wachezaji wao muhimu, ingawa kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kunaweza kupunguza mapato yao na kulazimisha maamuzi magumu.
Kocha wa Man United, Michael Carrick, alimpongeza Casemiro kwa mchango wake tangu alipowasili, aliposema: “Lazima niseme, Case amekuwa wa kipekee tangu nilipokuja ndani na nje ya uwanja. Uzoefu ni jambo kubwa kama utatumika kwa njia sahihi.”
Wachezaji wengine viungo waliotajwa kuhusishwa na Man United ni Carlos Baleba wa Brighton na Elliot Anderson wa Nottingham Forest.