Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Liverpool katika hali mbaya kabla ya msimu mpya

Muktasari:

  • Kuna matukio mawili makubwa yaliyobadilisha mwelekeo wa Liverpool linapokuja suala la mabeki.

LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL imeonywa kuwa inapaswa kumuunga mkono kocha wake mpya Andoni Iraola kwa kufanya usajili zaidi, baada ya kikosi hicho kuingia kwenye mgogoro mkubwa wa safu ya ulinzi huku msimu mpya wa Ligi Kuu England ukikaribia kuanza.

Kuna matukio mawili makubwa yaliyobadilisha mwelekeo wa Liverpool linapokuja suala la mabeki.

Majira ya joto yaliyopita, beki wa England Marc Guehi, alikuwa karibu kabisa kujiunga na Liverpool kiasi kwamba idara ya mawasiliano ya klabu yake ya zamani Crystal Palace ilikuwa tayari imeandaa video ya kumuaga kwa ajili ya mitandao ya kijamii. Video hiyo ilikuwa na picha zake akiwa ameinua Kombe la FA ikiwa na ujumbe wa "Asante Nahodha."

Hata hivyo, kama ilivyokuja kujulikana baadaye, dili hilo lilivunjika dakika za mwisho kabisa za siku ya mwisho ya usajili baada ya mwenyekiti wa Crystal Palace Steve Parish kulisitisha ghafla.

Kisha mwezi Aprili mwaka huu, Ibrahima Konate aliwaambia waandishi wa habari kuwa alikuwa karibu kusaini mkataba mpya na Liverpool.

Lakini miezi miwili baadaye, beki huyo Mfaransa aliaga Anfield na kufuata nyayo za Trent Alexander-Arnold kwa kuhamia Real Madrid akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake.

Sasa Liverpool imejikuta katika hali ngumu huku ikiwa imesalia wiki nne kabla ya enzi ya Andoni Iraola kuanza rasmi kwa mchezo dhidi ya Newcastle. Mechi hiyo pia itakuwa ya hisia kutokana na kifo cha gwiji wa vilabu hivyo viwili, Kevin Keegan.

Mwezi mmoja kabla ya msimu kuanza, Liverpool tayari inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa mabeki.

Kama mchezo wa kwanza ungechezwa kesho, nahodha Virgil van Dijk ndiye angekuwa beki pekee mwenye uzoefu anayepatikana. Hata hivyo, Mholanzi huyo bado hajaanza maandalizi ya msimu mpya baada ya kupewa mapumziko ya ziada kufuatia ushiriki wake katika Kombe la Dunia.

Joe Gomez, ambaye ameitumikia Liverpool kwa muda mrefu na ana uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali za ulinzi, alipata majeraha katika mchezo wa kwanza wa kirafiki wa maandalizi dhidi ya Sunderland uliochezwa Nashville nchini Marekani.

Iraola alisema hiyo ndiyo habari mbaya zaidi baada ya siku chache zilizopita kukiri kuwa kikosi chake kilikuwa "chepesi sana" katika eneo la ulinzi.

Ingawa Gomez anaheshimika sana ndani ya chumba cha kubadilishia nguo na kupendwa na mashabiki, ukweli ni kwamba mwili wake hauwezi tena kuaminika kutokana na majeraha ya mara kwa mara.

Takwimu za Transfermarkt, zinaonyesha kuwa hili ni jeraha lake la tisa tofauti tangu mwanzo wa msimu wa 2023/24.

Msimu uliopita alianza mechi saba za Ligi Kuu England, huku msimu uliotangulia akianza michezo sita pekee.

Bado haijajulikana ukubwa wa jeraha lake, lakini iwe atakaa nje kwa siku mbili au miezi miwili, hali ya Liverpool imekuwa wazi.

Mbali na Van Dijk na Gomez, Liverpool ina vijana wawili ambao inaamini ni miongoni mwa vipaji bora vya mabeki duniani.

Hata hivyo, wote wawili hawajawahi kucheza hata dakika moja katika Ligi Kuu England na kwa sasa pia wanauguza majeraha.

Jeremy Jacquet mwenye miaka 21, aliyesajiliwa kutoka Rennes kwa Pauni milioni 55 mwezi Januari, yupo nchini Marekani na kikosi lakini anasimamiwa kwa umakini mkubwa.

Kutokana na tatizo la bega lililomfanya asiichezee Rennes tangu Februari 7, Liverpool imeamua kumpa muda wa kutosha wa mazoezi kabla ya kumrudisha uwanjani.

Baada ya kukosa mchezo dhidi ya Sunderland, pia anatarajiwa kuukosa mchezo dhidi ya Wrexham jijini New York, huku akitarajiwa kucheza kwa mara ya kwanza dhidi ya Leeds mwishoni mwa wiki ijayo jijini Chicago.

Mlinzi mwingine ni Giovanni Leoni mwenye miaka 19 aliyesajiliwa kutoka Parma mwaka uliopita.

Kijana huyo wa Italia amekuwa nje ya uwanja kwa karibu mwaka mzima baada ya kupasuka mishipa ya goti (ACL) katika mechi yake ya kwanza mwezi Septemba.

Hata Jacquet na Leoni watakaporejea, bado hawana uzoefu wa kiwango cha juu na wangepaswa kupewa muda wa kuzoea taratibu.

Lakini kutokana na hali ilivyo sasa, huenda wakalazimika kutupwa moja kwa moja kwenye mechi kubwa.

Kutokana na matatizo hayo, vijana Mor Talla Ndiaye na Ifeanyi Ndukwe wamekuwa wakicheza nafasi hiyo katika mechi za maandalizi, huku Ndukwe akiwa bado hana kibali cha kufanya kazi na huenda akatolewa kwa mkopo msimu huu.

Van Dijk sasa ana miaka 35 na anaingia mwaka wa mwisho wa mkataba wake, hali ambayo pia inamhusu Gomez.

Ingawa Mholanzi huyo bado ni mmoja wa mabeki bora duniani, Liverpool haiwezi kuendelea kumtegemea milele.

Kutokana na hali hiyo, kusajili beki mpya sasa limekuwa jambo la kipaumbele sawa na kutafuta mrithi wa Mohamed Salah katika winga ya kulia.

Pia kuna matatizo safu ya ushambuliaji baada ya Hugo Ekitike kupata jeraha la kupasuka tendon ya Achilles, huku Alexander Isak akitarajiwa kukosa sehemu kubwa ya msimu kutokana na majeraha mbalimbali.

Msimu uliopita, Arne Slot alikosolewa kwa kiwango kikubwa licha ya kupewa zaidi ya Pauni milioni 450 kwa ajili ya usajili wa nyota kama Isak, Ekitike na Florian Wirtz.

Lakini sasa inaonekana Iraola amepewa kikosi ambacho bado kinakosa silaha muhimu za kufanikisha malengo makubwa ya Liverpool msimu huu.

Kocha huyo kutoka Hispania ameanza vizuri ndani ya klabu hiyo kwa namna alivyozungumza na pia alivyokiongoza kikosi katika mchezo wa kwanza wa kirafiki nchini Marekani.

Liverpool sasa ipo Chicago ambako imeungana na Florian Wirtz, Alexander Isak na Ryan Gravenberch waliokuwa wamepewa mapumziko baada ya kushiriki Kombe la Dunia.

Hata hivyo, kama Iraola hatapatiwa angalau wachezaji wawili au watatu zaidi kabla ya dirisha la usajili kufungwa, kocha huyo wa zamani wa Bournemouth anakabiliwa na kazi ngumu ya kuirejesha Liverpool kwenye mafanikio.

Wakati huo huo, taarifa zimeibuka kuwa bilionea wa Amazon Jeff Bezos ni sehemu ya kundi linalotaka kununua hisa za klabu hiyo zenye thamani ya Pauni bilioni 1.35.

Kwa hali ilivyo sasa, Liverpool inaonekana kuhitaji beki mpya kwa haraka zaidi kuliko wakati mwingine wowote.