Bernardo Silva, Barca wakaribia kumalizana
Muktasari:
- Silva tayari ametangaza kuwa ataondoka Man City mwishoni mwa msimu, jambo lililofungua njia kwa uhamisho wake kwenda Hispania.
BARCELONA wanakaribia kukamilisha dili la kumsajili kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya Ureno, Bernardo Silva, 31, kuelekea dirisha lijalo.
Silva tayari ametangaza kuwa ataondoka Man City mwishoni mwa msimu, jambo lililofungua njia kwa uhamisho wake kwenda Hispania.
Kiungo huyo awali alikuwa anahusishwa na vigogo wa Saudi Arabia ambao walikuwa tayari kuweka mezani ofa nono ili kumshawishi ajiunge nao lakini anadaiwa kukataa kwa sababu bado anahitaji kuendelea kucheza soka la kiushindani barani Ulaya.
Awali, Silva pia alikuwa katika rada za Juventus ya Italia lakini wababe hao wanaonekana kupunguza nguvu katika kuikimbizia saini yake hasa baada ya kuona Silva mwenyewe anatamani zaidi kujiunga na Barca badala ya timu nyingine.
Hata hivyo, licha ya kuonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kumsajili, Barca itatakiwa kuuza kwanza baadhi ya mastaa wake katika kikosi cha kwanza kabla ya kuingiza jina la Silva katika mfumo na kumwezesha kucheza La Liga, hiyo ni kutokana na ukomo wa kiasi cha mshahara ambacho wanatakiwa kulipa wachezaji kwa msimu mmoja kuwa kimeshafikiwa kwa sasa.
Tijjani Reijnders
JUVENTUS inadaiwa kuwa inaongoza katika vita ya kuiwania saini ya kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya Uholanzi, Tijjani Reijnders, 27, kuelekea dirisha lijalo majira ya kiangazi. Reijnders alijiunga na Man City msimu uliopita akitokea AC Milan kwa ada ya takribani Pauni 46.3 milioni lakini hajaonyesha kiwango bora kiasi cha kuhusishwa kutaka kurejea tena Serie A ambapo mbali ya Juventus, klabu nyingine ikiwemo Napoli na Inter Milan zimeonyesha nia ya kumsajili. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 45 za michuano yote na kufunga mabao saba. Mkataba wake unamalizika 2030.
Will Osula
KOCHA wa Newcastle United, Eddie Howe inadaiwa kutaka mshambuliaji wa Denmark, Will Osula, 22, aendelee kubaki St James’ Park msimu ujao. Osula amekuwa akiwindwa na klabu mbalimbali Ulaya na baadhi ya ripoti zilidai anaweza akaondoka dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Staa huyu mkataba wake unamalizika mwaka 2029, msimu huu amecheza mechi 32 za michuano yote na kufunga mabao saba. Mapema mwaka huu, baadhi ya tovuti zilidai Newcastle ilikuwa tayari kumuuza Osula Pauni 30 milioni.
Endrick
REAL Madrid inapanga kumbakisha mshambuliaji wao chipukizi wa kimataifa wa Brazil, Endrick, 19, msimu ujao licha ya klabu kubwa Ulaya zikiwamo Arsenal na Chelsea kuonyesha nia ya kutaka kumsajili. Endrick ambaye msimu huu anachezaa kwa mkopo Marseille ameonyesha kiwango bora kiasi cha kuzivutia timu hizo tajwa. Madrid inaamini atasaidia sana kikosi chao kwa siku za usoni, hivyo hawana mpango wa kumuuza kwa gharama yoyote.
Ross Barkley
KOCHA wa Coventry City, Frank Lampard anamtaka kiungo wa zamani wa England, Ross Barkley, 32, kuwa mchezaji wake wa kwanza kumsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Barkley anatarajiwa kumaliza mkataba wake Aston Villa mwishoni mwa msimu, hali inayomfanya kuwa chaguo rahisi kwa Converty ambayo imepanda daraja kucheza Ligi Kuu England msimu ujao. Lampard anaamini uzoefu wa Barkley Ligi Kuu England unaweza kuisaidia Coventry ambayo kundi kubwa la mastaa wake hawajawahi kucheza ligi hiyo.
Alex Remiro
REAL Sociedad inajaribu kumzuia kipa wao wa kimataifa wa Hispania, Alex Remiro, 31, asiondoke dirisha lijalo la majira ya kiangazi na vigogo wengi Ulaya wanataka kumsajili ikiwa pamoja na Barcelona. Barcelona wamekuwa wakimfuatilia Remiro kwa muda mrefu na wanaamini wakiipata saini yake atasaidia sana kuboresha na kuongeza ushindani golini. Kwa sasa Sociedad inapambana kuhakikisha inamsainisha mkataba mpya Remiro ambao utakuwa na maslahi mapana zaidi.
Konstantinos Mavropanos
BEKI wa kati wa West Ham United, Konstantinos Mavropanos, 28, anatarajiwa kuondoka dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Borussia Dortmund ndio inadaiwa imeonyesha nia ya kumsajili nyota huyo wa Ugiriki, lakini ina wasiwasi kuhusu gharama ya usajili ya nyota huyo. Kwa sasa mazungumzo yanaendelea na ripoti zinadai Mavropanos anatamani sana kuondoka kwenda Dortmund ili kupata changamoto mpya.
Teun Koopmeiners
MANCHESTER United imeanza mchakato wa kuwania saini ya kiungo wa kimataifa wa Uholanzi, Teun Koopmeiners, 28, anayekipiga Juventus.
Koopmeiners ni kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kucheza kama namba sita na nane na Juventus inaonekana kuwa tayari kumwachia dirisha lijalo lakini kwa klabu itakayotoa ofa inayoanzia Pauni 40 milioni. Kiasi hicho cha pesa kinaonekana kikubwa kwa timu zinazomhitaji, hivyo kwa sasa zinafanya mazungumzo na wawakilishi wa Juventus ili kupunguziwa bei.