Ben White alaumu mashabiki England
Muktasari:
- Baada ya tukio hilo, White alikataa kurejea kwenye kikosi cha England wakati Southgate na Holland wakiendelea kukinoa kikosi hicho. Hata hivyo, alirejeshwa kwenye timu na kocha Thomas Tuchel mwezi Machi mwaka huu.
LONDON, ENGLAND: BEKI wa Arsenal, Ben White, amesema mashabiki wa England wasingemzomea kama wangefahamu ukweli wote kuhusu sababu zilizomfanya aondoke kambini wakati wa Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.
White, ambaye aliondoka kwenye kikosi cha England baada ya hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa sababu binafsi, amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu tukio hilo lililoendelea kumuweka kwenye presha kutoka kwa mashabiki.
Wakati huo, taarifa zilidai kuwa beki huyo alikuwa na mgogoro na msaidizi wa aliyekuwa kocha wa England, Gareth Southgate, Steve Holland.
Baada ya tukio hilo, White alikataa kurejea kwenye kikosi cha England wakati Southgate na Holland wakiendelea kukinoa kikosi hicho. Hata hivyo, alirejeshwa kwenye timu na kocha Thomas Tuchel mwezi Machi mwaka huu.
Licha ya kurejea kwake, White alikutana na wakati mgumu mbele ya mashabiki wa England waliomzomea aliporejea uwanjani Wembley katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Uruguay.
Alipoingia kipindi cha pili, mashabiki walimzomea, lakini baadaye alifunga bao lake la kwanza akiwa na jezi ya timu ya taifa kabla ya kusababisha penalti dakika za mwisho, katika mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 29 hakuchaguliwa kwenye kikosi kilichoshiriki Kombe la Dunia lililofanyika Amerika Kaskazini, lakini sasa amerejea tena kwenye kikosi cha England kinachojiandaa na michezo ya Ligi ya Mataifa dhidi ya Croatia na Hispania.
Akizungumzia kwa mara ya kwanza kuhusu kitendo cha mashabiki kumzomea, White amesema ilikuwa vigumu kukabiliana na hali hiyo kwa sababu mashabiki hawakuwa na taarifa kamili kuhusu kilichotokea Qatar.
“Haikuwa rahisi kusikia wakinizomea, hasa kwa sababu hawakujua hali halisi iliyokuwepo. Hilo ndilo jambo ambalo nimekuwa nikiliweka akilini mwangu,” amesema White.
“Watu hawajui mazingira yangu na kiukweli si suala la kile nilichofanya, kwa sababu hawajui sababu zilizonifanya nifanye hivyo. Kama wangejua, naamini wasingenizomea wala kusema mambo yale. Nafikiri hawajui ukweli wote na kama wangeujua, pengine wasingenizomea.”
White ameongeza kuwa amekuwa akiona na kusikia taarifa mbalimbali kuhusu sakata hilo, lakini hana mpango wa kuweka wazi kila kitu kilichotokea wala kumlaumu mtu yeyote.
“Kuna mengi yamesemwa na huenda nimeona karibu kila kitu kilichoandikwa. Lakini nafikiri watu hawajui ukweli wote kwa sababu sijawahi kuzungumza kuhusu jambo hilo, na sitaki kumtupia mtu lawama au kumuweka mtu kwenye wakati mgumu kwa kueleza mambo hayo.
“Kulikuwa na mambo mengi yaliyotokea na mawasiliano hayakuwa mazuri. Sitaki kumlaumu mtu yeyote. Watu wengi wamekuwa wakijaribu kunifanya mimi ndiye mwenye makosa, lakini siwezi kufanya hivyo kwa mtu mwingine.
“Ni jambo gumu na si rahisi kulielezea, lakini ninafurahi kuwa hapa sasa. Ni heshima kubwa kuitwa kwenye kikosi cha taifa.”