Bellingham, Mbappe wailiza Barca El Clásico
Muktasari:
- Kiungo huyo wa timu ya taifa ya England, alipiga pasi ya kuvunja ngome ya ulinzi ya Barcelona na kumpasia Kylian Mbappé ambaye alifunga bao la kwanza dakika ya 22, kabla ya yeye mwenyewe kufunga bao la pili dakika ya 43, muda mfupi baada ya Fermin López kusawazisha dakika ya 38.
MADRID, HISPANIA: JUDE Bellingham amefunga na kutoa pasi ya bao kwa mara ya kwanza msimu huu wa La Liga wakati Real Madrid ikiibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Barcelona katika mechi ya El Clásico iliyojaa msisimko na hasira iliyochezwa kwenye Uwanja wa Bernabéu leo Jumapili Oktoba 26, 2025.
Kiungo huyo wa timu ya taifa ya England, alipiga pasi ya kuvunja ngome ya ulinzi ya Barcelona na kumpasia Kylian Mbappé ambaye alifunga bao la kwanza dakika ya 22, kabla ya yeye mwenyewe kufunga bao la pili dakika ya 43, muda mfupi baada ya Fermin López kusawazisha dakika ya 38.
Hilo lilikuwa bao la nne la Bellingham katika mechi tano za El Clásico, akisaidia kikosi cha Xabi Alonso kuongoza La Liga kwa pointi tano mbele ya Barcelona, huku mechi ikimalizika kwa Pedri kuonyeshwa kadi nyekundu na vurugu kutokea.
Real Madrid ilikuwa imepoteza mechi zote nne za El Clásico katika mashindano yote msimu uliopita, lakini safari hii iliianza mechi kwa kasi, ikijaribu mara kwa mara kuvunja safu ya juu ya ulinzi ya Barcelona.
Madrid ilidhani imepata penalti baada ya Vinícius Jr kuangushwa ndani ya dakika mbili za kwanza, lakini ukaguzi wa VAR ulionyesha kuwa winga huyo wa Brazil ndiye aliyemgonga Lamine Yamal kabla hajaanguka.
Dakika kumi baadaye, VAR ilifuta bao zuri la Mbappé aliyepiga shuti kali umbali wa yadi 25 kwa sababu ya kuotea kwa tofauti ndogo sana. Hata hivyo, Bellingham alimgeuza Pedri na kumpasia Mbappé pasi safi iliyomuwezesha kumfunga kipa Wojciech Szczęsny kwa utulivu.
Madrid iliendelea kushambulia lango la Barcelona, lakini ikashitukizwa dakika ya 38 kupitia shambulio la haraka lililoishia Marcus Rashford kumpasia Fermin López aliyesawazisha.
Lakini Real ilirejea mbele kabla ya mapumziko kwa mazingira yenye utata. Wachezaji wa Barcelona walilalamika kuwa beki Dean Huijsen alimkosa Pau Cubarsí wakati akiokoa mpira wa kichwa wa Éder Militão, lakini Bellingham alibaki peke yake upande wa pili na kufunga kwa urahisi.
Mbappé alifunga tena lakini bao lake likakataliwa kwa kuotea, baada ya ushirikiano mzuri wa pasi kati yake, Vinícius na Bellingham.
Kipindi cha pili kilianza kwa VAR kuingilia tena na kutoa penalti yenye utata kwa Real Madrid baada ya mpira kugonga mkono wa Eric García alipokuwa akijaribu kuokoa dhidi ya Bellingham.
Hata hivyo, Szczęsny alifanya uokoaji mzuri kwa mkono mmoja kuzuia penalti ya Mbappé katika dakika ya 52.
Dakika 20 kabla ya mechi kumalizika, Bellingham alifunga tena kutoka kwa krosi ya chini ya Brahim Díaz, lakini bao hilo pia likafutwa kwa sababu ya kuotea.
Barcelona ilishindwa kumpa kipa Thibaut Courtois majaribu makubwa, na mechi ikamalizika kwa vurugu kati ya benchi za timu zote mbili.
Hasira zililipuka zaidi baada ya Pedri kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kufuatia kumchezea vibaya Aurélien Tchouaméni katika muda wa majeruhi.
Ushindi huo umeifanya Real Madrid kujitanua zaidi kileleni mwa msimamo wa La Liga ikifikisha pointi 27, ikiiacha Barcelona kwa pointi tano kwani inazo 22, zote zikishuka dimbani mara kumi.