Atletico yatua kwa Alejandro Garnacho
Muktasari:
- Garnacho mwenye umri miaka 20, mechi nyingi amekuwa akiingia akitokea benchi na msimu huu amefunga mabao manane katika mechi 24 alizocheza.
ATLETICO Madrid inataka kumsajili winga wa Manchester United, Alejandro Garnacho ambaye ameonekana kutokuwa katika vipaumbele vya kocha Ruben Amorim tangu achukue mikoba ya kuifundisha timu hiyo.
Garnacho mwenye umri miaka 20, mechi nyingi amekuwa akiingia akitokea benchi na msimu huu amefunga mabao manane katika mechi 24 alizocheza.
Staa huyu kutoka Argentina alikosekana pia katika mechi iliyopita dhidi ya Manchester City ambapo hakusafiri kabisa na timu na Amorim alisema alimwacha kwa sababu hakuridhishwa na baadhi ya mambo yake ikiwamo mazoezi.
Simeone amekuwa akitamani sana kumsajili Muargentina mwenzake huyu na sasa inaonekana kuwa ndio nafasi ya kufanikisha hilo. Mkataba wa Garnacho unaisha 2028.
LIVERPOOL inaweza kusitisha mpango wao wa kutaka kumsajili mshambuliaji wa Brighton, Joao Pedro katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi mwakani ikiwa itafanikisha mchakato wa kumsainisha mkataba mpya Mohamed Salah.
Salah ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, awali alionekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kuondoka lakini sasa mazungumzo yanaenda vizuri na kuna asilimia nyingi kwmaba anaweza kubaki. Mkataba wake unaisha 2028.
MSHAMBULIAJI wa Atalanta na Nigeria, Ademola Lookman ambaye hivi karibuni ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika, yupo katika orodha ya timu mbalimbali za England ikiwamo Arsenal na Manchester United zinazohitaji kumsajili katika dirisha lijalo.
Lookman, mmoja kati ya mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Atalanta, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2026. Msimu huu amecheza mechi 17 za michuano yote na kufunga mabao 10.
REAL Betis imefikita patamu katika mazungumzo yake na Madrid ili kuipata saini ya kiungo wa Real Madrid na Hispania, Dani Ceballos, 28, katika dirisha dogo la usajili Januari 2025.
Ceballos ambaye hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Madrdi, mkataba wake na wababe hao unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Msimu huu amecheza mechi nane za michuano yote.
KOCHA wa AS Roma ametoa ruhusa ya mshambuliaji wa timu hiyo Paulo Dybala kuondoka katika timu hiyo kwenye dirisha lijalo la majira ya baridi ikiwa hana furaha.
Tayari wawakilishi wa Dybala wameshaanza mchakato wa kumtafutia staa huyo timu mpya ambapo wamekutana na mabosi wa Galatasaray kwa ajili ya mazungumzo juu ya kutua timu hiyo mwezi ujao.
MANCHESTER United ipo katika hatua nzuri kwenye mazungumzo ya kumuongeza mkataba mpya staa wao raia wa Ivory Coast, Amad Diallo ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu. Vigogo wa United wanahitaji huduma ya fundi huyu kutokana na kiwango bora alichoonyesha. Msimu huu amecheza mechi 23 za michuano yote, amefunga mabao manne na kuasisti sita.
EVERTON inataka kumsajili straika wa Rangers na Morocco, Hamza Igamane katika dirisha lijalo kwa ajili ya kuboresha eneo la ushambuliaji ambalo huenda likaondokewa na Dominic Clevert Lewin na Beto mwisho wa msimu. Hamza ameonyesha kiwango bora tangu msimu uliopita ambapo alicheza mechi 23 za michuano yote na kufunga mabao saba.
EVERTON imepanga kumsajili winga wa Olympique Lyon na Ghana, Ernest Nuamah, 21, katika dirisha la majira ya kiangazi mwakani.
Ernest mwenye umri wa miaka 21, ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Lyon na msimu huu amecheza mechi 14 za michuano yote na kufunga bao moja.