Atletico, Barca na Liverpool vitani kufuzu nusu fainali UEFA
Muktasari:
- Mchezo huo sambamba na ule wa Liverpool wanaoikaribisha PSG wakiwa na deni la mabao 0-2, ni mechi ambazo zinatazamiwa kuhanikiza anga la vita ya ubabe katika mashindano hayo msimu huu na nyota wa vikosi hivyo wanatarajia kupambana kuhakikisha wanatoka viwanjani wakicheka.
MADRID, HISPANIA: KUNA kila sababu katika usiku wa Ulaya leo, Atletico Madrid na Barcelona zitashuka katika Uwanja wa Wanda Metropolitano kuamua nani atatinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, baada ya wiki iliyomaliza wababe wa LaLiga, Barca kuambulia kichapo cha mabao 2-0 nyumbani.
Mchezo huo sambamba na ule wa Liverpool wanaoikaribisha PSG wakiwa na deni la mabao 0-2, ni mechi ambazo zinatazamiwa kuhanikiza anga la vita ya ubabe katika mashindano hayo msimu huu na nyota wa vikosi hivyo wanatarajia kupambana kuhakikisha wanatoka viwanjani wakicheka.
Ingawa kinachotazamiwa huenda kukawa na maajabu, lakini kinachoonekana katika makaratasi huenda kikabakia kuwa kilekile kwani timu zilizopoteza wiki iliyopita yaani Barcelona na Liverpool zimekuwa na matokeo ya panda shuka katika mashindano hayo msimu huu, zikiwa hazina mwendelezo mzuri wa ushindi.
Hata hivyo, tofauti na Barcelona inayoongoza katika msimamo wa LaLiga kwa tisa dhidi ya Real Madrid inayokamata nafasi ya pili, Liverpool imekuwa na mwenendo usioridhisha Ligi Kuu England ikiwa na rekodi mbovu zaidi katika siku za karibuni ikikamata nafasi ya tano na pointi 52.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England wameendelea kutokuwa na uhakika wa ushindi wanaposhuka viwanjani katika mashindano mbalimbali msimu huu, kwani hata katika ligi mechi ambazo wamekuwa wakiangusha alama zimekuwa ni zile za kushangaza ambapo kuna wakati wanatangulia kufunga, lakini wanaishia kupoteza.
Kwa upande wa Barcelona, msimu huu kabla ya mechi iliyopita iliichapa Atletico Madrid mabao 2-1 ugenini na hivyo ikizichanga vyema karata zake inaweza kulipiza kisasi leo, hivyo kutinga nusu fainali ya mashindano hayo.
Mechi nyingine mbili za robo fainali zinapigwa kesho ambapo Real Madrid watakuwa ugenini katika Dimba la Allianz Arena kukipiga na Bayern Munich katika mchezo ambao mabingwa hao wa msimu juuu wa Ligi Kuu Hispania watakuwa na kazi ya ziada kujibu mapigo baada ya kuchapwa 2-1 nyumbani katika Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Ushindi wa Bayern haukuwapa tu faida kwenye jumla ya matokeo, bali pia ulimaliza kipindi kirefu cha kukwama dhidi ya Madrid, ambapo walishindwa kushinda katika mechi tisa mfululizo iliyopita. Kilicho muhimu zaidi ulikuwa ushindi wao wa kwanza katika uwanja wa Santiago Bernabeu ndani ya miaka 25. Mara ya mwisho Bayern waliposhinda ilikuwa 2000-01 katika nusu fainali, waliposhinda mechi zote mbili njiani kuelekea kunyanyua ubingwa.
Sasa, chini ya kocha Vincent Kompany, Bayern wana nafasi ya kurudia mafanikio hayo kwani wamekuwa na rekodi bora wanapolinda ushindi wa mchezo wa kwanza walioupata ugenini. Katika Ligi ya Mabingwa pekee wamefanikiwa kufuzu hatua inayofuata mara 21 kati ya 22 katika mazingira hayo.
Tukio pekee waliloshindwa lilikuwa 2010-11 dhidi ya Inter Milan, ambapo sheria ya bao la ugenini (ambayo sasa imeondolewa) iliwagharimu licha ya kushinda 3-2 katika mchezo wa marudiano.
Mbali na historia, Bayern wanaweza pia kutegemea ubora wao wa sasa wakiwa nyumbani, ambapo wameshinda mechi zote tano za nyumbani, wakifunga mabao 16 na kuruhusu matatu.
Mchezo mwingine kesho utakuwa kati ya Sporting CP watakapotua Emirates kukipiga na Arsenal, wakikumbuka kipigo cha bao 1-0 nyumbani kwao. Huu huenda mchezo mwingine wenye maajabu kutokana na ubora wa timu hizo na pia wageni waliotoka kushinda 4-2 katika Ligi Kuu Ureno (Primeira Liga), ilhali wenyeji wao wakipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Bournemouth katika Ligi Kuu England. Nani kutinga nusu fainali? Dakika 90 zitaamua!