Aston Villa yatia mguu kwa Sancho

Muktasari:
- Sancho ambaye amechana na Chelsea aliyokuwa anaichezea kwa mkopo msimu uliopita, hataki kuendelea kusalia katika kikosi cha kwanza cha Man United na badala yake anataka kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine.
ASTON Villa imeingia katika harakati za kutaka kumsajili winga wa Manchester United na England, Jadon Sancho, 25, katika dirisha hili.
Sancho ambaye amechana na Chelsea aliyokuwa anaichezea kwa mkopo msimu uliopita, hataki kuendelea kusalia katika kikosi cha kwanza cha Man United na badala yake anataka kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine.
Benchi la ufundi la Villa limevutiwa na kiwango ambacho staa huyu amekionyesha kwa msimu uliopita ambako alifunga mabao matano katika mechi 42 za michuano yote.
Mkataba wa sasa wa Sancho unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Mbali na ofa ya Villa, inaelezwa pia Juventus pia inaitamani saini yake.
Hapo awali, alicheza katika za vijana za klabu za Watford na Manchester City.
Sancho alisaini mkataba wake wa kwanza wa kucheza soka la watu wazima akiwa na Borussia Dortmund mwaka 2017.
Katika misimu minne akiwa na Dortmund, alicheza mechi 137 na kushinda DFL-Supercup mwaka 2019 pamoja na DFB-Pokal ya msimu wa 2020–21, ambapo alimaliza akiwa mfungaji bora wa mashindano hayo.
Sancho alirejea England na kusaini na Manchester United mwaka 2021, ambako alishinda Kombe la Carabao (EFL) katika msimu wake wa pili.
Baadaye alirejea Dortmund kwa mkopo, na kusaidia klabu hiyo kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2024 na kisha kutua Chelsea alikoenda kwa mkopo.
James Trafford
NEWCASTLE United imemweka kipa wa Burnley raia wa England, James Trafford kwenye orodha ya wachezaji inaotaka kuwasajili katika dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya.
Mabosi wa Newcastle wanataka huduma ya Trafford kwa ajili ya kuboresha safu yao ya ulinzi kuelekea msimu ujao ambapo watacheza michuano ya kimataifa.
Luis Diaz
INAELEZWA Liverpool haina nia ya kumuuza winga wa Colombia, Luis Diaz, mwenye umri wa miaka 28, na hadi sasa haijapokea ofa yoyote licha ya ripoti kudai kwamba anawindwa na Barcelona na Al-Nassr ya Saudi Arabia.
Mkataba wa Diaz unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Msimu uliopita winga huyo alicheza mechi 50 za michuano yote na kufunga mabao 17. Anasemekana kuipenda Barca tangu utotoni.
Anthony Gordon
MABOSI wa Liverpool wanaangalia uwezekano wa kumsajili winga wa Newcastle United, Anthony Gordon, mwenye umri wa miaka 24, kuelekea dirisha hili la majira ya kiangazi.
Gordon ambaye msimu huu amecheza mechi 42 za michuano yote na kufunga mabao tisa, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Benjamin Sesko
ARSENAL ipo katika vita kali dhidi ya Liverpool kwa ajili ya kuiwania saini ya mshambuliaji wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, 22, katika dirisha hili.
Ripoti za awali zinaeleza kwamba Arsenal tayari imeshawasilisha ofa kwa ajili ya kumsajili staa huyu inayokadiriwa kufikia Pauni 67 milioni. Katika msimu uliopita Sesko alifunga mabao 21 katika mechi 49 za michuano yote.
Thierno Barry
EVERTON imeambiwa kuwa italazimika kulipa Euro 40 milioni ili kuvunja mkataba wa mshambuliaji wa Villarreal, Thierno Barry katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Kiasi hicho cha pesa kipo katika mkataba wa staa huyo kwa timu yoyote itakayotaka kumnunua. Msimu uliopita alicheza mechi 41 za michuano yote na kufunga mabao 19.
Mike Maignan
CHELSEA haiko tayari kulipa Pauni 25 milioni ambazo AC Milan inahitaji kwa ajili ya kumuuza kipa wao raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 29, Mike Maignan katika dirisha hili.
Mabosi wa Chelsea wanahitaji sana huduma ya Maignan kwa ajili ya kuboresha eneo lao la lango baada ya Roberto Sanchez kutoonyesha kiwango bora kwa msimu uliopita.
Raphael Onyedika
WEST Ham wamewasiliana na Club Brugge kuhusu mpango wa kumsajili kiungo wa kati wa Nigeria, Raphael Onyedika (24), lakini inakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa AC Milan.
Onyedika ni miongoni mwa wachezaji tegemeo walioonyesha kiwango bora msimu uliopita. Msimu uliomalizika amecheza mechi 52 za michuano yote.