Amorim apewa mbinu kuinusuru Man United
Muktasari:
- Mechi tano za Amorim kwenye kikosi cha Man United zimekuwa na mchanganyiko wa mambo, akishinda mbili mfululizo dhidi ya Bodo/Glimt na Everton na kufuatia vichapo vingine viwili mbele ya Arsenal na Nottingham Forest huku mechi yake ya kwanza kabisa dhidi ya Ipswich Town ilimalizika kwa sare.
LONDON, ENGLAND: NDO hivyo. Kocha Ruben Amorim ameambiwa aangalie tu wachezaji wanaofiti kwenye mtindo wake wa uchezaji ili kunusuru hali ya mambo kwenye kikosi cha Manchester United, anafichua Chris Sutton.
Mechi tano za Amorim kwenye kikosi cha Man United zimekuwa na mchanganyiko wa mambo, akishinda mbili mfululizo dhidi ya Bodo/Glimt na Everton na kufuatia vichapo vingine viwili mbele ya Arsenal na Nottingham Forest huku mechi yake ya kwanza kabisa dhidi ya Ipswich Town ilimalizika kwa sare.
Kwa sasa wachezaji wa Man United bado wanapambana kujaribu kumudu fomesheni pendwa ya kiuchezaji ya kocha Amorim, 3-4-3 huku wakishika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, pointi nane nyuma ya Top Four.
Jambo hilo linamfanya kocha huyo mpya kutokuwa na muda wa kutosha kuweka mambo yake sawa na usiku wa leo Alhamisi kikosi hicho cha Man United kitakabiliwa na mechi ya Europa League dhidi ya Viktoria Plzen itakayofuatiwa na Manchester Derby dhidi ya Manchester City, Jumapili.
Amorim amekuwa akibadili mara kwa mara kikosi chake kwa wiki za karibuni, akijaribu kumpa nafasi kila mchezaji, jambo ambalo Sutton amedai litamgharimu kwenye matokeo ya mechi zake.
“Kikombe chake hakina kitu, hakina hata majina matatu,” alisema Sutton wakati alipoulizwa achague wachezaji watatu wenye uhakika wa kupata namba kikosi cha kwanza cha Amorim.
“Fomesheni ya 3-4-3, kuicheza, kwenye mechi tatu ndani ya wiki moja ni kazi ngumu sana. Haikunishangaza mimi, mtihani wa kwanza ulikuwa kwenye kucheza mipira ya kutenga ya Arsenal. Kisha, wikiendi iliyopita kwenye mechi dhidi ya Forest, ambao wamekuwa na msimu mzuri. Walikuwa na wakati mgumu na ukweli sijaona kitu kikubwa kilichobadilika. Huyu ni kocha aliyekuja, ambaye anahitaji uvumilivu ili kuandaa kitu kizuri.
“Kama mnavyojua, kuna mambo sio rahisi. Hili si tatizo lake. Tatizo ni amerithi kikosi na anajaribu kusafisha mambo na kuweka vitu sawa.
“Nadhani Bruno Fernandes – anaweza kutafuta nafasi na kufanya kitu. Siku zote namfikiria Lisandro Martinez ana kitu na Kobbie Mainoo. Nina wasiwasi na (Christian) Eriksen na Casemiro kama wataweza kudumu kwa muda mrefu kama watacheza kwa mtindo unaochezwa kwa sasa kwa sababu inahitaji miguu yenye nguvu ya kukimbia muda wote. Mainoo ana kitu cha ziada kuliko uwezo wa miguu yake kwenye kukimbia. Wachezaji wengine wapo tu na nimefurahi hamkutaka nitaje wachezaji watano.”
Man United ipo tayari kufanya mabadiliko na mshambuliaji Marcus Rashford ni mmoja wa wachezaji ambao wamewekwa sokoni kwa timu zitakazohitaji huduma yao kweye dirisha la Januari. Mmiliki mwenza wa klabu ya Man United, bilionea Sir Jim Ratcliffe amepanga kukifumua na kukijenga upya kikosi hicho na viungo kama Casemiro na Eriksen watafunguliwa mlango wa kutokea mwishoni mwa msimu, wakati Harry Maguire, Victor Lindelof na Jonny Evans nao wanaweza kupewa mkono wa kwaheri wakati dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa Juni mwakani.
Amorim anaamini atapata kikosi bora kabisa kutoka kwa wachezaji aliowarithi kutoka kwa mtangulizi wake Erik ten Hag endapo atapewa muda.
“Yapasa uendelee kufanya kazi yako, kufanya kitu kilekile, ukiwa na imaani kwamba kitakwenda kweye njia zako,” alisema Amorim baada ya kichapo kutoka kwa Nottingham Forest.
“Nashawishika kwenye hilo. Inauma kupoteza mechi. Nafahamu jamii na mashabiki wanataka ushindi. Imechukua muda mrefu bila ya kushinda na kuwa na hizo hisia za ushindi. Tupo kwenye safari ndefu, lakini tutafika.”