Mayombya, Camara wamkuna Mkenya
Muktasari:
- Camara ambaye ni kiungo mshambuliaji kutoka Guinea aliyejiunga na timu hiyo msimu uliopita akitokea Singida Black Stars kwa mkopo, huku Mayombya akisajiliwa dirisha dogo msimu uliopita kutoka Tanzania Prisons.
NYOTA Yonta Camara raia wa Guinea na Zabona Mayombya ni miongoni mwa wachezaji waliomkuna Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza aliyetaja kinachowabeba kikosini kiasi cha kuwafanya kuwa tegemeo msimu huu.
Camara ambaye ni kiungo mshambuliaji kutoka Guinea aliyejiunga na timu hiyo msimu uliopita akitokea Singida Black Stars kwa mkopo, huku Mayombya akisajiliwa dirisha dogo msimu uliopita kutoka Tanzania Prisons.
Akiwazungumzia mastaa hao, Baraza ambaye raia wa Kenya amesema ni wachezaji muhimu wanaojua kazi zao na maeneo ya kujipanga uwanjani na kwamba muda wowote wanaweza kufanya jambo kwa ajili ya timu.
Akimzungumzia Mayombya ambaye ni msumbufu kwa mabeki wa timu pinzani, amesema nyota huyo ni kati ya viungo bora Ligi Kuu ndio maana alipopata majeraha timu ilihangaika katika baadhi ya mechi.
“Naweza kusema nilikuwa nimekosa mtu maana’ke Zabona anajitengenezea sehemu ya kucheza na ukiangalia pia umri wake na hauwezi kupeleka sehemu nyingine ili uweze kumtumia. Huyu jamaa sehemu fulani anayoipatia akipiga chenga moja, mbili tatu yupo golini,” amesema Baraza na kuongeza:
“Katika mechi tatu tulizocheza bila Zabona na baadhi ya wachezaji wengine waliokuwa na majeraha ndiyo maana hatukuwa na matokeo mazuri pia bahati hakuwa yetu.”
Kuhusu kiungo mshambuliaji Yonta Camara, kocha huyo amesema mchezaji huyo anatoa msaada mkubwa kwa timu akiwa uwanjani kwani hakai kwenye nafasi moja pekee jambo ambalo linamvutia kwani ni mpenzi wa wachezaji wa aina hiyo.
“Mimi kama kocha naona akiwa ndani ananipatia msaada gani. Siku zote nawaambia vijana wangu tumuangalie Yonta akiwa anakuja hapa mwingine aingie hapa na imekuwa ikifanyika hivyo na inatupa matokeo mazuri,” amesema Baraza.
Licha ya Baraza kuwasifia nyota hao hadi sasa hakuna aliyefunga bao wala kuasisti, huku timu hiyo ikiwa nafasi ya tatu kupitia mechi sita ikivuna pointi tisa zikiwamo tatu za mezani kutoka kwa Dodoma Jiji.