Zimamoto yazidi kutamba Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Katika mechi nyingine, Mlandege ilikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa KVZ, mabao yaliyofungwa na Yakoub Said '6' na Akram Muhina '87'.
BAADA ya Zimamoto kuwasulubu mabaharia KMKM kwa mabao 2-1, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdallah Mohamed 'Bares' amesema ushindi huo ulipatikana kwa mpango wa kuzuia maeneo ya mpinzani yake.
Amesema kipindi cha kwanza timu hiyo ilikosa nafasi nyingi ndiyo sababu ya kubadilisha mkakati kwa kipindi cha pili ambao ulizaa matunda.
"Kipindi cha pili tuliingia na gemu plani ya kuzuia maeneo yao na ndiyo sababu ya kupata matokeo mazuri," amesema na kuongeza, eneo la beki bado halipo vizuri kwa timu hiyo hivyo ipo haja ya kulitafutia ufumbuzi kwa lengo la kutoharibu mbele ya safari.
Vile vile, kocha huyo amesema kikubwa anachohitaji kiongezeke kwa timu hiyo ni umiliki wa mpira wa muda mrefu kwani ndivyo namna timu inafanya vizuri kwa kutengeneza nafasi na kuzifikia kwa haraka zaidi.
Kocha huyo amesema KVZ ina kazi kubwa ya kufanya kuwashawishi mashabiki kufika uwanjani kuwapa hamasa.
Mbali na hilo, Bares aliwapa pongezi wachezaji wa KMKM kwa kucheza vizuri na kukubali kipigo cha mabao hayo kutoka kwao kwani mpira una matokeo matatu.
Mabao katika mechi hiyo yalifungwa na Hussein Maulid dakika ya 13 na Rashid Said dakika 90+1 huku la KMKM likifungwa na Haji Makame '65'.
Katika mechi nyingine, Mlandege ilikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa KVZ, mabao yaliyofungwa na Yakoub Said '6' na Akram Muhina '87'.