ZILITRENDI: Wawili Simba wazuiwa Nigeria

KAMA kawaida ya Alhamisi ukurasa huu, huwa unaangalia stori zilizobamba miaka ya nyuma, lakini katika tarehe husika na leo tunaenda hadi mwaka 2008.
Katika tarehe kama ya leo yaani Machi 24 ya mwaka huo, Simba ikiwa inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ilisafiri kwenda Nigeria kwa ajili ya pambano lao dhidi ya Enyimba lililopigwa Machi 23, 2008, huku ikijikuta wachezaji wake wawili wakizuiwa.
Wachezaji hao, Ramadhan Wasso na Mosses Odhiambo walizuiwa kuingia Nigeria pamoja na kikosi cha Simba kutokana na kukosa viza za kuingilia nchini humo.
Wasso, ni raia wa Burundi na Odhiambo ni Mkenya na wote walizuiwa katika uwanja wa ndege wa Lagos kutokana na kukosa viza, licha ya maofisa wa Idara ya Uhamiaji ya Lagos kuombwa sana na viongozi wa Simba ili waingie kuwahi pambano hilo.
Wachezaji hao walilazimika kubaki mjini Lagos kwani viongozi walioambatana na timu hiyo pamoja na baadhi ya wanachama wa kundi la Friends of Simba walikuwa wakifanya juhudi kubwa ili wachezaji hao waruhusiwe kuingia Nigeria.
"Wasso na Odhiambo hati zao za kusafiria (pasipoti) zilikuwa uhamiaji jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata vibali, lakini tulizipata pasi hizo wakati timu inajiandaa kuondoka wakati huo ubalozi wa Nigeria nchini Tanzania ulikuwa umefungwa," alisema mmoja wa viongozi wa Simba aliyeongeza;
"Tuliwachukua wachezaji hao na kusafiri nao tukiamini tutapata viza zao uwanja wa ndege wa Lagos kama inavyowezekana kwenye mechi nyingine za Afrika."
Hadi jioni ya jana ambako mchezo dhidi ya Enyimba ulipigwa mjini Aba, wachezaji hao walikuwa bado wamezuiwa uwanja wa ndege wa Lagos huku juhudi kubwa zikifanywa na Serikali ya Tanzania na Nigeria japo ilishindikana na kugeuza ndege kurejea Dar.
Katika mchezo huo, Simba ilinyooshwa mabao 4-0 na iliporudiana tena na Enyimba jijini Dar es Salaam Aprili 5, 2008 walipigwa tena mabao 3-1 na kutolewa kwa jumla ya mabao 7-1.