Zahera awashtukia Yondani, Makambo Yanga
YANGA imetua mkoani Morogoro na wameanza ratiba yao kamili ya mazoezi lakini kocha Mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera ameiangalia safu yake ya ushambuliaji na ile ya ulinzi kisha akawapa jukumu moja mabosi wake.
Akizungumza na Mwanaspoti Zahera amesema ameiangalia safu yake ya ushambuliaji na kushtuka kwamba licha ya kumpata Heritier Makambo bado wanahitaji straika mwingine haraka wa kigeni.
Zahera alisema endapo mabosi wake wataweza kupiga kazi ya maana kwa kumletea straika mwingine wa kigeni safu yake ya ushambuliaji itakuwa imekamilika kwa namna anavyohitaji.
Mbali na straika huyo kocha huyo raia wa DR Congo alisema nafasi nyingine anayohitaji mtu wa haraka wa kusajiliwa ni beki wa kati atakayekuwa na ubora kama wa Kelvin Yondani.
Alisema Yondani anahitaji kupata mtu wa kumpa changamoto kuwania nafasi ili kuleta ushindani wakati Andrew Vincent 'Dante akipambana na Abdallah Shaibu 'Ninja'.
Ameomba kama atapatikana beki wa kulia au kupata beki wa kati atakayeweza kucheza nafasi ya beki wa kulia kuziba nafasi ya Hassan Ramadhan 'Kessy' aliyetimkia Nkana FC ya Zambia.
"Nimeambiwa bado kuna muda kidogo wa kusajili wachezaji wa kigeni sasa ukiangalia kikosi chetu tunahitaji straika mwingine bora kama Makambo,"alisema Zahera.
"Hilo nimewakabidhi viongozi pia kama watapata beki wa kati mmoja mwenye ubora kama Kelvin (Yondani) basi tutakuwa tumeboresha nafasi hiyo, nataka mtu wa kushindana na Kelvin (Yondani) pia unajua Kessy hatakuwepo ni vyema tukapata beki wa kulia atakayeshindana na Juma (Abdul).
"Ili uwe na timu nzuri inayoshindana ni vyema kila nafasi ukawa na watu wawili au zaidi ili ushindani uwepo ukiacha mtu mmoja ni rahisi mchezaji kubweteka na kuiangusha timu."