Zahera apewa mashine mpya
Muktasari:
- Aliliambia Mwanaspoti kuwa alimkabidhi Zahera majina ya Patrick Kaddu na Umar Kasumba.
KIPA Mkenya Farouk Shikalo amekutana kwa mara nyingine tena na bosi wake mtarajiwa nchini Misri, Mwinyi Zahera lakini safari hii kukiwa na usiri mkubwa.
Awali, wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza nchini Ufaransa ambako timu ya Taifa ya Kenya ilikuwa imepiga kambi kujiandaa na Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), huku Zahera akiwa na kikosi chake cha DR Congo, ambapo wenyewe waliweka kambi kule Hispania.
Hata hivyo, Mwanaspoti ambalo limeweka kambi kwenye Jiji la Cairo, Misri lilinasa kikao hicho cha siri na miongoni mwa yaliyojiri ni Shikalo kumkabidhi Zahera majina ya mastraika wawili tishio.
Shikalo, ambaye yuko kwenye hatua za mwisho kukamilisha dili la kutua Yanga, amemkabidhi Zahera majina hayo na kumweleza kwamba kama atawanasa basi msimu ujao kwenye Ligi Kuu Bara na ile ya kimataifa, Yanga itakuwa moto.
Baada ya Mwanaspoti kunasa tarifa hizo lilimsaka Shikalo ambaye yuko jijini hapa akiwa na timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars, ambapo alikiri kukutana na Zahera huku akisema kilikuwa kikao cha kawaida.
Lakini, akafichua kwamba ni kweli alimkabidhi Zahera majina mawili ya mastraika hao Waganda akimuomba awasajili kama si wote, basi hata mmoja.
Aliliambia Mwanaspoti kuwa alimkabidhi Zahera majina ya Patrick Kaddu na Umar Kasumba.
Kaddu ndiye aliyewafunga DR Congo bao la kwanza wakati timu ya Taifa ya Uganda ‘The Craines’ ikishinda mchezo wake wa kwanza kwenye fainali hizo.
Katika mchezo huo The Craines ilishinda mabao 2-0 huku Kaddu anayekipiga KCCA ya Uganda, akifunga bao la kwanza kwa kichwa kuunganisha mpira wa kona.
Kwa upande wake, Kasumba ndiye mshambuliaji tegemeo kwenye kikosi cha Sofapaka (Batoto ba Mungu) kinachoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL).
Hata hivyo, Shikalo alimpongeza Zahera kwa kufanya usajili wa straika wa Polisi ya Uganda, Juma Balinya akisema Yanga imelamba dume kwani Mganda huyo ni hatari anapokaribia lango la adui.
“Nimekutana na mwalimu na amezungumza mambo mengi, lakini nilimweleza mawazo yangu kuhusu washambuliaji wawili wa Uganda ambao nawafahamu vizuri. Wanacheza Ligi Kuu Kenya.
“Pale Kenya kuna mtu anaitwa Umar Kasumba anachezea Sofapaka, huyu anajua sana kuwasumbua mabeki na juzi hapa Misri nimemuona huyu aliyewafunga Congo bao la kwanza anaitwa Kaddu (Patrick) ni mzuri sana.
“Ila kocha ameniambia kuwa atalifanyia kazi hilo japo tayari mabosi wake wamemsajili mshambuliaji aliyeongoza kwa ufungaji pale Uganda, nadhani na huyo atakuwa bora zaidi kwa rekodi hiyo.
“Kwa upande wangu niko vizuri na tutamalizana na Yanga muda si mrefu, kwa sasa nataka hizi fainali zimalizike kwani nimeamua kutafuta changamoto nyingine. Nahitaji kuondoka Kenya kwa sasa,” alisema Shikalo
Rekodi za Kaddu
Mshambuliaji wa kati, Patrick Henry Kaddu raia wa Uganda, alizaliwa Oktoba 9, 1993 nchini humo na sasa ana miaka 23.
Yuko chini ya wakala Hassan Amzil na sasa anakipiga katika Klabu ya KCCA aliyojiunga nayo Julai 2017.
Kabla ya KCCA kwa mujibu wa mtandao, Kaddu alianza kucheza soka la ushindani akiwa na Klabu ya Kiira Young FC ya Uganda aliyojiunga nayo Julai 1, 2015.
Kaddu ni miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha ‘The Cranes’.
Katika msimu wa 2016/2017 amekuwa mfungaji bora akitupia wavuni mabao 16.
Rekodi za Kasumba
Straika Umar Kasumba alizaliwa Februari 9, 1994 na sasa ana miaka 25 akiwa na uzito kilo 72.
Raia huyo wa Uganda anaichezea Sofapaka ya nchini Kenya na pia ni miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’
Kabla ya kujiunga na Sofapaka katika msimu wa 2014/2015, Kasumba aliichezea Police Jinja, 2015/2016 Villa Kampala na mwaka 2017 alijiunga na Sofapaka anayoichezea mpaka sasa.