Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yazuia usajili wa Sh.4 bilioni za Merreikh

Mshambuliaji wa timu ya Yanga Kenneth Asamoah (mbele) akijaribu kuwatoka mabeki wa timu ya El-Merreikh wakati wa mechi ya kombe la Kagame iliyofanyika juzi jumapili kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

MWANDISHI WETU LICHA ya kuanza benchi katika mechi dhidi ya Yanga, Stephen Worgu wa El Merreikh ya Sudan ana thamani kuliko wachezaji wote wa Tanzania. Usajili wa Worgu kutoka Enyimba kwenda El Merreikh uliwagharimu Waarabu hao Sh.bilioni nne za Tanzania. Usajili wa Yanga na Simba tu kwa pamoja haufiki Shilingi bilioni moja, lakini Worgu mwenye umri wa miaka 20, thamani yake ni shilingi bilioni nne. Usajili wa wachezaji wote wa klabu 16 za Ligi Kuu Bara, kwa makadirio ya juu sana, unaweza kufika Shilingi bilioni mbili. Worgu, ambaye ni raia wa Nigeria anafahamika vizuri nchini kwani alikuja na Enyimba mwaka 2008 na kumtungua Juma Kaseja mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Worgu anayevaa jezi namba kumi alianza benchi katika mechi dhidi ya Yanga juzi Jumapili kabla ya kuingia kipindi cha pili. AKIMBIA VITA LIBYA Worgu ambaye alizaliwa Aprili 6, mwaka 1990 ni Mnigeria ambaye El Merrikh ilimpeleka kwa mkopo katika klabu ya Al-Ahly Benghazi SC ya Libya mwaka jana. Alicheza Libya kuanzia Septemba 15, mwaka jana mpaka Juni 15 mwaka huu aliporejea El Merreikh kutokana na kukimbia vita inayoendelea sasa nchini humo. FEDHA TENA Klabu hiyo ya Libya ilimlipa Worgu dola 300,000 (Sh. milioni 450) huku El Merreikh ikilipwa dola 200,000 (Sh.milioni 300). ALIKOANZA Worgu amewahi kuchezea Ocean Boys ya Nigeria kuanzia mwaka 2005 mpaka 2007 na walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Nigeria. Julai, 2007, Worgu alijiunga na Enyimba, ambayo alikaa nayo mwaka moja na anakumbukwa jinsi alivyokuja nayo Dar es Salaam Mei, 2008 kucheza na Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Mwaka 2008, Worgu aliiongoza Enyimba kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku yeye akiwa mfungaji bora wa mashindano hayo kwa kufunga mabao 13 akimzidi Daouda Kamilou wa Cotonsport Garoua aliyefunga mabao manane. FEDHA ZA WAARABU KIBOKO Oktoba 22, 2008, Worgu alikubali kusaini mkataba wa miaka minne wa kuchezea El Merreikh, ambayo ndio timu tajiri zaidi Sudan na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. El Merreikh ilimpa mkataba huo Worgu na kuipiku Al Ahly ya Misri na timu nyingine kubwa za Afrika ambazo zilikuwa zinamgombea. Mkataba wa mchezaji huo ulikuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 2.5 (Shilingi bilioni 4 za Tanzania). Enyimba ililipwa dola za Marekani milioni 1.5 sawa na Shilingi bilioni 2.4 za Tanzania, huku dola milioni moja yaani Sh bilioni 1.6 za Tanzania akipewa Worgu mwenyewe. Worgu inadaiwa kuwa alikubali ofa hiyo ya El Merreikh kutokana na ofa kubwa, lakini alikuwa ni Mnigeria wa tatu kucheza soka Sudan wengine wakiwa ni Isahor na Osunwa. Akiwa El Merreikh alipewa jezi namba 10 na kuachana na jezi namba 27 aliyokuwa akiitumia alipokuwa Enyimba. Hata hivyo, mambo hayakuwa mazuri kwake kwani katika mechi saba za mwanzo na El Merreikh alishindwa kufunga bao lolote kwenye Ligi Kuu Sudan, huku akishindwa kufunga katika mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika. Aprili 23, 2009 walipokuwa wakicheza dhidi ya Al Ittihad katika Ligi Kuu Sudan alipewa kadi ya njano dakika za mwanzo za mchezo, na alipofunga bao alishangilia kwa kuvua jezi hivyo kupewa kadi ya pili ya njano iliyosababisha apewa nyekundu. El Merreikh ilishinda 2-0. AHUKUMIWA VIBOKO 40 Agosti, 2009, Worgu alishikwa na polisi kwa kosa la kunywa pombe jambo ambalo ni kinyume na sheria za Sudan, lakini klabu yake ya El Merreikh ilimlipia faini ya pauni milioni 24, alihukumiwa pia kupigwa viboko 40. Kutokana na kiwango chake kushuka Septemba mwaka jana alipelekwa kwa mkopo katika klabu ya Al Ahly Benghazi ya Libya kabla ya kurudishwa Juni mwaka huu kutokana na vita inayoendelea. Katika mchezo wa juzi Jumapili dhidi ya Yanga, aliingia kipindi cha pili lakini hakuwa na makali zaidi ya kutoa pasi ya bao la pili.