Prime
Yanga yavamia ‘jeshini’
YANGA inaendelea kufanya usajili wa kuboresha kikosi hicho, ikichanganya wachezaji wazoefu na chipukizi na tayari inadaiwa ipo kwenye mazungumzo ya mwisho na kinda Suleiman Mbarouk kutoka JKU ya Zanzibar.
Mbarouk anayejulikana kama Mpemba D ana umri wa miaka 18, ameahidiwa mkataba wa miaka mitatu kuitumikia klabu ya Yanga.
Mbarouk anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji atakwenda kukutana na ushindani wa namba katika kikosi cha Yanga ambapo kuna Allan Okello, Maxi Nzengeli, Pacome na endapo usajili wa Aziz KI ukikamilika pia anacheza eneo hilo.
Chanzo cha ndani kutoka JKU kilisema Yanga imepeleka maombi ya kumtaka mchezaji huyo na ipo tayari kununua mkataba wake ambao ulisalia wa mwaka mmoja, wakiamini kipaji chake watakiendeleza.
“Tumemalizana na Yanga na mchezaji ameandaliwa mkataba wa miaka mitatu, tunaamini atapata nafasi ya kujifunza zaidi akijituma kwa bidii ni daraja lake la kufika mbali,” kilisema chanzo hicho.
Siyo mara ya kwanza kwa Yanga kusajili wachezaji kutoka Zanzibar kwa miaka ya hivi karibuni imefanya hivyo kwa Shekhan Ibrahim Khamis walimtoa JKU na sasa amepelekwa kucheza Singida Black Stars kwa mkopo, mwingine ni kiungo mkabaji Abdulnasir Abdallah ‘Casemiro’ alisajiliwa kwa miaka mitatu kutoka Mlandege ya Zanzibar.
Msimu huu klabu zimeruhusiwa kusajili wachezaji 40 kwa ajili ya mashindano.