Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo matatu ya Kelvin Nashon

NASHON Pict


KWA ushuhuda wa macho yangu kiungo ambaye Simba wamemsajili kutoka Pamba ya Mwanza, Kelvin Nashon ni mzuri na bora kuliko kiungo ambaye Simba wamekuwa naye akitoka nje ya nchi, Alissane Kante. Nazungumza kwa mujibu wa macho yangu.


Nashon ana mambo mengi mazuri uwanjani. Lakini matatu muhimu Anakaba, anapiga pasi, anajiamini. Ana tatizo moja tu. Kuna wakati anazidisha kucheza kwa nguvu zaidi na anajikuta anacheza rafu. Hajui muda gani wa kufika katika mwili wa mpinzani au muda gani ajizuie. Basi. Hana matatizo mengine.


Ananifurahisha hili la upambanaji. Ni wale wachezaji mashujaa. Ni wale wachezaji washindani haswa uwanjani. Juzi Simba wamemtangaza kama mchezaji wao na nikakiri moyoni kwamba wamepata mchezaji mzuri.

Hata hivyo, nafsi inanisuta kwa sababu nimewahi kusema hivi mara nyingi kwa wachezaji wa aina ya Nashon. Unamtabiria makubwa halafu anakuangusha. Unamfikiria mbali lakini anakuangusha.

Hiki ndio ambacho kimesababisha tujaze wachezaji wengi wa kigeni katika ligi yetu. Hiki ndicho ambacho kimesababisha wachezaji wa kigeni waonekane muhimu katika klabu zetu kuliko wachezaji wazawa. Kuna mahala ambapo wachezaji wazawa hawatimizi wajibu wao.

NASHO 02

Aliwahi kuniambia staa wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Sunday Manara. Niliwahi kumuuliza kwanini wachezaji wa siku sio bora kuliko wao akanijibu kwamba tofauti ni wao walikuwa wanacheza katika asilimia mia ya ubora wao wakati wachezaji wa siku hizi wanacheza asilimia 40 tu ya ubora wao.

Wachezaji wengi mahiri wazawa ambao waliingia katika hizi timu zetu kubwa za Simba, Yanga na Azam wametuangusha. Wakifika katika klabu hizi unaona wanacheza chini ya kiwango au katika kiwango kilekile. Hawasogei mbele. Hawashindani.

Huyu Nashon anapishana na wachezaji kadhaa wadogo ambao walisajiliwa Simba katika miaka ya karibuni huku kukiwa na matarajio makubwa kwao. Ladack Chasambi, Edwin Balua na Kelvin Kijili. Wote tuliamini kwamba wanakwenda kutoboa pale Msimbazi. Kilichotokea wote tunakijua.

Leo Balua, Chasambi na Kijili wote wamepewa mkono wa kwaheri. Kukuta wachezaji wapya wazawa wakiingia katika timu moja kwa moja ni ngumu. Maeneo ambayo yanatusumbua sana ni kuanzia katika kiungo kwenda mbele.

NASHO 04

Kuwakuta wachezaji kama Yusuf Kagoma, Mudathir Yahaya, Clement Mzize na wachache wengineo wakiingia moja kwa moja katika vikosi vya wakubwa huwa ni nadra. Orodha ya walioshindwa ni kubwa.

Kuna jambo linawakuta wachezaji wetu wakiingia katika hizi timu. Wengine wanabweteka, wengine huwa wanacheza kwa kutetemeka, wengine huwa wanashindwa kujifunza na kujifua zaidi.

Usidhani waliowasajili akina Baraka Mwangosi na Emmanuel Mwanengo ni wajinga. Hapana. Kuna kitu walikiona katika miguu yao wakahisi kwamba wanaweza kuwa ‘Mzize mpya’. Imeshindikana. Nadhani wote watatolewa kwa mkopo katika dirisha hili.

Kwa macho yangu Nashon ni mchezaji bora kuliko Kante lakini mwisho wa msimu unaoanza hivi karibuni utatupa majibu mazuri. Atamudu presha ya kucheza Simba kwa ubora ule ule ambao amekuwa akiufanya katika timu nyingine?

Lakini pia wakati nikiamini kwamba Nashon ni bora kuliko Kante, kwanini sasa Kante yupo nchini na Nashon yupo hapa hapa? Hii ndio tofauti ya wachezaji wa Afrika Magharibi na sisi. Wao wanahangaikia maisha lakini sisi tunazisubiri Simba na Yanga.

NASHO 05

Nashon alikuwa anazisubiri Simba, Yanga au Azam. Angeamua kuondoka zake sidhani kama ligi kuu ya Misri ingemshinda. Anacheza katika staili ile ile ya Himid Mao Mkami ambaye alitamba Misri lakini yeye alikuwa anazisubiri Simba na Yanga.

Kante amehangaika nje ya taifa lake la Senegal na amejikuta akiangukia Tanzania. Sisi huwa tunaangukia hapa hapa. Haishangazi kuona wachezaji wetu hawaisaidii Taifa Stars. Wengi wanasubiri kucheza Simba na Yanga.

Kila la kheri kwa Nashon. Kama yeye na Kagoma watakuwa moto zaidi basi watakuwa wameipunguzia Simba matumizi yasiyo ya lazima katika eneo la kiungo wa chini ambapo wakubwa wetu wamekuwa wakilazimika kusaka mchezaji wa kigeni kila kukicha.

Katika nafasi hiyo hiyo, Jonas Mkude alikuwa akibadilishiwa wachezaji wengi wa kigeni. Kuanzia wakati ule wa Fraga na wengine waliokuja Mkude alikuwa analazimika kushirikiana na mgeni mmoja. Kwa sasa nadhani hesabu zinaonyesha kuwa lile eneo la chini Kagoma na Nashon watakuwa wazawa wawili wanaoweza kujitanua zaidi.

Katika hesabu za kiuchumi ni kwamba Simba watalazimika kutia pesa katika maeneo mengine muhimu ya uwanja. Ni kama ambavyo katika miaka ya karibuni pesa yao ambayo wangezamisha kwa wachezaji wa kigeni katika eneo la ulinzi wa pembeni zimeokolewa na wachezaji wazawa. Akina Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Nickson Kibabage, David Kameta ‘Duchu’ na wengineo.

Ni kama ambavyo watani wao wameokolewa sana katika matumizi ya pesa kwa kigeni katika nafasi ya ulinzi wa kati. Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto na Dickson Job wamekuwa wakifanya kazi nzuri kiasi kwamba ni ngumu kwa mgeni kupata nafasi Jangwani.

Baada ya msimu ujao kumalizika tutakuwa katika nafasi nzuri ya kujua kama Nashon ameokoa pesa za Simba katika eneo hilo. Kwa mtazamo wangu ni kiungo mzuri kuliko viungo wa chini ambao Simba na Yanga iliwaleta katika miaka ya karibuni. Mzuri kuliko Kante, Balla Conte na Mohamed Damaro.

Tatizo la wachezaji wetu wakifika katika hizi timu hawajitambui. Wanawalazimisha mabosi wa hizi timu kuamini kwamba suluhisho bora ni kuleta watu wa maana kutoka nje. Kwa sasa kiungo wa maana wa mitaa ya chini ambaye unakiri kwamba anastahili kulipwa pesa za kigeni ni Duke Abuya. Yupo pale Jangwani. Anazima dimba lake.