Yanga yarejea kileleni ikiipiga JKT Tanzania 4-0
Muktasari:
- Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi tisa ikitoka nafasi ya tatu na kurudi juu ya msimamo ikifunga jumla ya mabao 11 katika mechi tatu ilizocheza, huku ikiruhusu mawili.
YANGA imeendeleza ubabe dhidi ya JKT Tanzania ikiichapa mabao 4-0, huku mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wakiendeleza mwanzo bora wa msimu wa 2026-2027.
Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi tisa ikitoka nafasi ya tatu na kurudi juu ya msimamo ikifunga jumla ya mabao 11 katika mechi tatu ilizocheza, huku ikiruhusu mawili.
Yanga leo imetengeneza nusu ya mabao ambayo iliyafunga dhidi ya JKT msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara ambapo wanajeshi hao waliruhusu mabao nane kwenye mechi mbili walizokutana.
Februari 25, 2026, JKT ilipokea kipigo cha mabao 5-0 kabla ya kufungwa tena 3-0 ikiwa kwao, Juni 30, 2026, ikiwa moja ya timu ilizopoteza kwa mabao mengi msimu uliopita.
Yanga leo imejihakikishia ushindi huo mapema tu ndani ya dakika 45 za kwanza ikipata mabao yake matatu yakifungwa na Albert Kangwanda dakika ya 28, Ibrahim Abdulla 'Bacca' dakika ya 34 kwa kichwa, kisha Chadrack Boka akipiga la tatu dakika ya 39 wenyeji wakionyesha ubabe kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Kipindi cha pili, Yanga ikapata bao la nne dakika ya 64 kupitia mshambuliaji Peter Shalulile kwa kichwa akimalizia krosi ya Kangwanda.
Bao hilo linakuwa la pili kwa Shalulile katika mechi tatu, huku Kangwanda akiendeleza moto akifikisha pia mabao mawili huku akitengeneza mawili na kumfanya mpaka sasa kuhusika kwenye jumla ya mabao manne, leo akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo. Chadrack Boka naye amefikisha mabao mawili, akiwa pia na asisti mbili.
JKT haikuwa na maajabu mbele ya Yanga kwani haikutengeneza mashambulizi mengi ambapo nafasi pekee ambayo itajutiwa na wanajeshi hao ni ile ya dakika 50 wakati mshambuliaji wake, Paul Peter akiwa yeye na kipa wa Yanga, Djigui Diarra alishindwa kukamilisha jaribio lake la kutaka kumpiga chenga na kupokonywa mpira.
Kipigo cha leo kinaifanya JKT Tanzania mechi tatu kuambulia pointi moja baada ya kutoka 1-1 nyumbani dhidi ya TRA United, kisha ikafungwa 2-0 na Polisi Tanzania na kichapo cha 4-0 kutoka kwa Yanga.