Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yapeleka jezi ya bahati CAF

YANGA juzi ilizindua jezi zake itakazozitumia katika mashindano ya kimataifa lakini uzinduzi huo umekuja na mabadiliko ambayo imeyafanya ikiamini yanaweza kuwa chachu ya kufanya vizuri katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika linalosimamiwa na Caf.
Mabadiliko hayo ni ya kutumia jezi zenye rangi nyeusi kwa mechi za nyumbani za mashindano hayo huku mechi za ugenini wakipanga kutumia jezi za kijani na jezi yenye rangi ya njano ikitumika kama ya tatu (third kit), iwapo watakutana na mazingira ambayo yatawafanya washindwe kutumia jezi za nyumbani au ugenini.
Mwanaspoti imethibitishiwa kuwa Yanga tayari imeshatuma taarifa kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), ikiwajulisha kuhusu jezi itakazozitumia katika hatua ya makundi na zile za juu iwapo itafanikiwa kupenya kwenda robo fainali na nusu fainali.
"Ni jezi ambazo tumekuwa na bahati nazo pindi tunapozitumia hivyo tumeamua katika mashindano ya kimataifa msimu huu, mechi za nyumbani tutatumia jezi nyeusi na ugenini tutavaa jezi za rangi ya kijani. Lakini kama mazingira yataruhusu hata huko ugenini, tutavaa jezi za rangi nyeusi na tumeshawapa taarifa Caf kwa mujibu wa kanuni," kilifichua chanzo hicho cha uhakika.
Tangu walipovaa jezi za rangi nyeusi walipoibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Club Africain ya Tunisia kwenye mechi ya marudiano ya hatua ya mwisho ya mchujo ya Kombe la Shirikisho Afrika na kufuzu hatua ya makundi baada ya suluhu ya hapa nchini, Yanga imekuwa na mwendelezo wa kuzitumia jezi zenye rangi hiyo kwa mechi nyingi za mashindano ya ndani ziwe za nyumbani au ugenini ikiwa pia ndiyo jezi yao kipenzi kwenye Ligi Kuu Bara.
Baada ya mchezo huo wa ugenini dhidi ya Club Africain, Yanga imecheza mechi 17 za mashindano tofauti ambapo katika hiyo, michezo 10 ilicheza ikiwa imevaa jezi nyeusi na kupata ushindi yote ikifunga mabao 20 na kuruhusu bao moja tu, jezi za rangi ya kijani wamechezea mechi sita ambazo wameshinda zote wakifunga mabao 21 na kufungwa mabao matatu huku jezi ya njano wakichezea mechi moja na walipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu.
Hivi karibuni kulikuwa na gumzo kubwa kuhusu jezi hiyo lakini Yanga wanaamini kuwa ndiyo inabahati kwenye michezo yao, jezi ya Caf imeboreshwa na ina tofauti kubwa na ile ambayo mashabiki wameizoea, huku ikiwa na ubora wa juu zaidi.
Baada ya Yanga kuichapa Rhino mabao 7-0 kwenye mchezo wa ASFC watacheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo Februari 4 na baada ya hapo itasafiri kwenda Tunisia kuvaana na Monastir kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Shirikisho Afrika