Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yapata mchekea CAF

Muktasari:

  • Hatua hiyo inaweza kuwa faida kwa Wanajangwani ambao sasa watacheza mechi zote mbili katika mazingira ya nyumbani, endapo ombi hilo litathibitishwa rasmi.

YANGA imepata mserereko wa mapema kabla ya kukutana na CFFA ya Madagascar katika hatua ya pili ya mchujo wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya wapinzani hao kuomba mchezo wao wa nyumbani uchezwe Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Hatua hiyo inaweza kuwa faida kwa Wanajangwani ambao sasa watacheza mechi zote mbili katika mazingira ya nyumbani, endapo ombi hilo litathibitishwa rasmi.

Awali, CFFA ilitumia Uwanja wa kutoka nchini Mauritania katika mchezo wake wa mchujo wa kwanza, lakini sasa imeomba kutumia Azam Complex kwa pambano lake dhidi ya Yanga.

Akizungumza kuhusu suala hilo, Meneja wa Azam Complex, Amiry Juma, amethibitisha kupokea barua ya maombi kutoka kwa klabu hiyo ya Madagascar na kueleza kuwa tayari wameijibu.

“Tulipokea barua yao na tumeshawajibu. Kama si leo au kesho tutathibitisha ujio wao,” alisema Juma.


REKODI ZA YANGA KIMATAIFA

Yanga inaingia katika hatua hiyo ikiwa na rekodi ya kucheza mechi mbili za mchujo wa kwanza msimu huu wa 2026/2027 dhidi ya Gaborone United ya Botswana, ikitoka sare ya bao 1-1 ugenini kabla ya kushinda mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano.

Matokeo hayo yaliifanya Yanga kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2 na sasa kukutana na CFFA, ambayo nayo ilifuzu baada ya kuiondoa Lijabatho ya Lesotho kwa jumla ya mabao 3-1.

Kwa mujibu wa ratiba za CAF, mchezo wa kwanza kati ya Yanga na CFFA umepangwa kuchezwa Jumamosi Oktoba 17, 2026 huku marudiano yakitarajiwa Oktoba 24, 2026.

Sasa macho ya Wanajangwani ni kuona kama ombi la CFFA litakubaliwa rasmi, jambo linaloweza kuifanya Yanga kuwa na mazingira inayoyafahamu katika michezo yote miwili ya kuwania nafasi ya kwenda hatua ya makundi.