Prime
Yanga ilivyotegua mitego Isamuhyo, yanusa harufu ya dhahabu
YANGA imegoma kupoteza mchezo wa pili mbele ya Simba ikilazimisha sare ya mabao 2-2, baada ya matokeo hayo bosi wao mmoja wa juu akafichua namna walivyokwepa mitego kwenye dabi hiyo huku akisema sasa wanaufuata ubingwa.
Timu hizo zimemalizana msimu huu kwenye ligi zikiwa hakuna iliyopoteza zilipokutana, zikianza kutoka 0-0, kisha sare ya 2-2, huku pia kila moja ikitamba kushinda mashindano mengine. Yanga ilishinda Ngao ya Jamii kwa bao 1-0, Simba ikaja kulipa kwa kubeba Kombe la Muungano ikiichapa Yanga 1-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo alisema haikuwa rahisi kwa timu hiyo kupata matokeo hayo dhidi ya Simba wakilazimika kutegua mambo mengi.
Gumbo alisema kila kitu kilichofanyika kwa timu hiyo uwanjani hapo kilikuwa na hesabu kali na kikosi chao kilistahili ushindi baada ya kutegua mitego mingi endapo tu mwamuzi wa mchezo huo Hamza El Fareq kutoka Morocco angekuwa makini.
"Tumepata sare, tunamshukuru Mungu lakini kiukweli tulistahili kushinda, tulifanya kazi kubwa ya kutegua mambo ambayo kwetu tunaona kama ilikuwa ni mitego ambayo ililenga tupoteze hii mechi," alisema Gumbo.
"Hatua ya kufanikiwa mitego hiyo ambayo kwetu itabaki kuwa siri ndio ilifanikisha timu yetu kuingia uwanjani na ubora mkubwa, tulikuwa na ubora kwa wachezaji wetu wa kurudisha hata mabao matatu achana na hayo mawili.
"Tulikuwa tunatamani maamuzi makini tu, kama mwamuzi angekuwa makini tulikuwa tunashinda hii mechi ya jana (juzi) kulikuwa na maamuzi ambayo yalitunyima nafasi za kupata mabao na watu wote wameona."
Aidha Gumbo aliongeza kuwa, baada ya dabi hiyo kumalizika, sasa Yanga inajipanga kwenda kumalizia mechi zilizosalia kwa kishindo ili kutetea ubingwa wa ligi.
Alisema kikosi cha timu hiyo bado kipo kwenye ubora kikiendelea kulinda heshima ya kutopoteza mchezo wowote kwenye ligi katika mechi 20 ilizocheza mpaka sasa.
"Tumebakiza mechi 10 kumaliza ligi na timu yetu imeendelea kuonyesha tabia ya timu bingwa ambazo huwa siyo rahisi kukubali kupoteza, tunakwenda kuchukua tebna ubingwa.
"Unapomaliza mechi kubwa kama hizi bila kupoteza, pia tukiendelea kuwa moja kati ya timu mbili ambazo hazijapoteza mechi yoyote msimu huu hii ni ishara tupo sawasawa," alisema.
DUBE ATIA NENO
Wakati Gumbo akiyasema hayo, mshambuliaji kinara wa ufungaji ndani ya timu hiyo na ligi akiwa sambamba na Feisal Salum wa Azam, Prince Dube aliongeza akisema sio rahisi timu hiyo kukubali kipigo mara mbili mfululizo.
"Hii ni Yanga, hata kama tutaanguka lakini hatuwezi kukubali matokeo mabaya kirahisi, tuna nguvu ya kuinuana na kuendelea na vita mpaka tufanikiwe na huu ndio mwendo wetu," alisema Dube mwenye mabao tisa Ligi Kuu Bara.
ADHABU YAWASUBIRI
Katika mechi hiyo, kuna matukio ya nje ya uwanja ambayo kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu 2025, bila shaka kuna adhabu ambayo Yanga itakumbana nayo.
Yanga itakumbana na adhabu baada ya watu wake kuonekana wakimwaga maji eneo la goli na inatafsiriwa kama mambo ya imani za kishirikina. Kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu, adhabu yake ni faini ya Sh5 milioni.
Kosa lingine ni kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na badala yake Yanga ilitumia nyumba iliyokuwa pembeni mwa uwanja huo.
Kufanya hivyo ni kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo ambapo adhabu yake ni faini ya Sh5 milioni tano.