Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga bana! Yaangusha moja moja

Wachezaji wa yanga wakishangilia jambo katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam

MWANDISHI WETU KATIKA mechi nne zilizopita, Yanga imekuwa ikishinda kwa bao moja moja, lakini Kocha Ernie Brandts amesema hakuna tatizo ingawa wikiendi iliyopita aliwapangua mastraika wake. Yanga ni vinara wa Ligi Kuu Bara ambao wanaongoza wakiwa na pointi 48 na wanafuatiwa na Azam FC yenye 37 na Simba 34. Ndani ya mechi nne mfululizo wameshinda kwa ushindi finyu wa bao moja moja kuanzia walipocheza na Azam FC 1-0, Kagera Sugar 1-0, Toto Africa 1-0 na Ruvu Shootings 1-0 na sehemu kubwa ya mabao hayo yamefungwa na viungo. Brandts alisema: "Si mbaya sana kwa sababu kikubwa tunaondoka na pointi tatu muhimu,"alisema Brandts, ambaye amewataka washambuliaji wake kubadilika. Mshambuliaji pekee aliyeanza katika mchezo uliopita ni Hamis Kiiza ambaye ndiye aliyefunga bao la ushindi huku Jerrson Tegete, Didier Kavumbagu na Said Bahanuzi wakiwekwa benchi na Nizar Khalfan ambaye ni kiungo akichezeshwa kama mshambuliaji wa kati. Kiiza alisema: "Kukosa nafasi za kufunga kwa washambuliaji huwa inatokea, lakini tunaamini tutafunga mabao mengi zaidi kubwa tuvumiliane, tunashinda lakini nitaridhika zaidi pale tutakapochukua ubingwa, sasa bado kabisa kwa sababu tuna mechi mbele yetu na hatujui matokeo." Nizar alicheza sambamba na Kiiza lakini hata hivyo Nizar aliumia dakika ya 80 na hivyo Kavumbagu kuchukua nafasi yake. "Nimemuanzisha Nizar kwa sababu ameonyesha kubadilika na kucheza vizuri katika mechi nilizompanga, anajituma sana na kila mmoja ameona, washambuliaji wangu wanatakiwa kuyafanyia kazi makosa yao na kujitahidi wanapopata nafasi ya kucheza kwani ushindi ni mabao,"alisisitiza Kocha Brandts. Bahanuzi, ambaye aliibuka mfungaji bora kwenye michuano ya Kagame mwaka jana, amepoa ghafla msimu huu ingawa benchi la ufundi linadai majeruhi yamechangia huku Tegete aliyeibuka kwa kasi siku za karibuni kwa kufunga karibu kila mechi akipotea katika mechi nne mfululizo kwa kutofunga bao lolote. Kavumbagu, ambaye alianza msimu vizuri na kumaliza mzunguko wa kwanza akiwa na mabao nane sawa na Kipre Tchetche wa Azam amejikuta akipotea katika mechi nyingi za mzunguko wa pili na hadi sasa katika mzunguko huo ametupi bao moja tu ingawa amekuwa akiwataka mashabiki wa Yanga kutulia mambo mazuri yanakuja. Ali Mustapher 'Barthez' ambaye ni kipa namba moja wa Yanga, ameiambia timu yake ya zamani wa Simba kwamba wala wasijisumbue na ubingwa na sasa watafute cha kufanya kupata nafasi pili ambayo wanawania na Azam. Barthez anamini pointi 14 walizowaacha Simba hawawezi hata kidogo kutia mguu na kuwafikia ; "Hao Simba wanahangaika tu lakini kutukamata ni ndoto wapambane kutafuta nafasi ya pili lakini hata wakiomba tupoteze mechi hicho kitu hakiwezi kutokea,tumewaacha mbali sana hivyo ubingwa msimu huu ni wetu," ambaye tangu ajiunge na Yanga hajaitwa Taifa Stars licha ya uhodari wake langoni. Yanga imesaliwa na mechi sita kumaliza msimu na tatu itazicheza ugenini na tatu jijini Dar es Salaam. Machi 30, itakuwa Morogoro kucheza na Polisi ya huko kabla ya kurudi Dar es Salaam kukabiliana na JKT Oljoro Aprili 10 na baadaye Aprili 13 itaenda Tanga kuivaa Mgambo JKT. Aprili 21 watacheza na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, baadaye Mei Mosi itakuwa Tanga kwa Coastal Union na kabla ya kumalizana na Simba ndani ya Uwanja wa Taifa Mei 18 kufunga msimu wa 2012/13.