Wavu Zanzibar kutafutiwa udhamini
NAIBU Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Ali Abdulghulam Hussein, amesema wizara hiyo ipo tayari kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Wavu Zanzibar kutafuta wadhamini.
Amesema, endapo mchezo huo utapata udhamini wa uhakika, utakuwa na uwezo wa kuendeleza mchezo huo kwa lengo la kuongeza ushindani miongoni mwa timu zilizopo.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa michezo katika kukuza ajira, vipaji vya vijana na uchumi, hivyo itaendelea kutoa ushirikiano kwa vyama vyote vya mchezo vilivyopo Zanzibar.
Amebainisha kuwa mojawapo ya changamoto zinazowakabili ni ukosefu wa wadhamini unaowaweka katika wakati mgumu, hali inayowafanya baadhi ya wanamichezo kuona kucheza mchezo mwingine kaipambele sawa na mpira wa miguu.
“Moja ya changamoto kubwa zinazoikabili Mashirikisho mengi Zanzibar ni kutokuwa na udhamini kwenye michezo yao, jambo ambalo linawawia ugumu kuendesha mashindano ya ndani,” amesema.
Ameahidi kuwa wizara itaendelea kushirikiana na mashirikisho yote kutafuta wadhamini mbalimbali ili kuwasaidia wanamichezo kwani Serikali pekee haiwezi kugharamia mahitaji yote ya mchezo.