Siku 17 za mapumziko kwa Kagera Sugar
Muktasari:
- Ligi hiyo inatarajiwa kusimama kuanzia Novemba 3, 2026 hadi Novemba 20, 2026 kupisha kalenda ya FIFA ambapo kitatumika kuchezwa mechi za kufuzu AFCON 2027, kipindi ambacho Kaze anakiona kama fursa ya kutosha kutathmini upungufu uliojitokeza katika michezo iliyopita, hasa namna timu yake inavyoruhusu mabao na kushindwa kutumia nafasi inazotengeneza.
KOCHA wa Kagera Sugar, Cedric Kaze amesema siku 17 za mapumziko ya Ligi Kuu zitakuwa muhimu kwake katika kufanya marekebisho ya kikosi chake baada ya kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Yanga, akibainisha maeneo ambayo anahitaji kuyafanyia kazi ili timu irejee ikiwa imara zaidi.
Ligi hiyo inatarajiwa kusimama kuanzia Novemba 3, 2026 hadi Novemba 20, 2026 kupisha kalenda ya FIFA ambapo kitatumika kuchezwa mechi za kufuzu AFCON 2027, kipindi ambacho Kaze anakiona kama fursa ya kutosha kutathmini upungufu uliojitokeza katika michezo iliyopita, hasa namna timu yake inavyoruhusu mabao na kushindwa kutumia nafasi inazotengeneza.
Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Yanga, Kaze amesema mapumziko hayo yatampa nafasi ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza, akisisitiza kuwa eneo la ulinzi linahitaji kufanyiwa kazi zaidi kutokana na idadi ya mabao ambayo wamekuwa wakiruhusu.
Kagera Sugar ndio timu iliyoruhusu mabao mengi msimu huu ikifungwa 22 kwenye mechi 11 ilizocheza ikipata ushindi mechi moja, sare tatu na kupoteza saba na ikisalia mkiani. “Ni kweli tutapata muda mzuri wa kujiandaa pia kukosoa vitu ambavyo tunaamini haviko vizuri; sana hasa kwenye eneo la kuruhusu magoli mengi, inabidi hivyo vitu kuvirekebisha katika hizi siku,” amesema Kaze.
Kocha huyo ameongeza kuwa mbali na eneo hilo pia ana kazi ya kuongeza makali ya washambuliaji, hasa katika kufanya uamuzi sahihi wanapofika maeneo ya mwisho.
Kaze alikiri kuwa timu hiyo imekuwa na uwezo wa kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma kwa pasi fupi, lakini inakwama katika hatua ya mwisho.
“Katika kushambulia tulikuwa tunaanzisha vizuri mashambulizi kuanzia nyuma, tukitumia pasi fupi fupi na kuweza kufika katika maeneo ya mwisho ya uwanja, lakini tulikosa kufanya maamuzi sahihi na umakini katika utekelezaji wa mipango yetu,” amefafanua kocha huyo.
Eneo lingine litakalohitaji umakini ni nidhamu ya kiuchezaji na umakini wa wachezaji kwa dakika zote 90, kwani kwa mtazamo wa Kaze, makosa madogo dhidi ya timu zenye ubora mkubwa yanaweza kuigharimu timu yake.