Wanajeshi wamehamishia vita kwa kinda Alliance
Muktasari:
- Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka kwa chanzo cha ndani zinaeleza Mashujaa Queens tayari imewasilisha ofa kwa Alliance Girls, lakini bado hawajafikia dau walilolitaka.
TIMU za Jeshi, JKT Queens na Mashujaa Queens zimeingia kwenye vita ya kusaka saini ya kiungo mshambuliaji, Noadia Robert baada ya kuonyesha kiwango bora msimu uliopita.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka kwa chanzo cha ndani zinaeleza Mashujaa Queens tayari imewasilisha ofa kwa Alliance Girls, lakini bado hawajafikia dau walilolitaka.
Inaelezwa JKT imeweka ofa ambayo bado timu hiyo inandelea kuichambua na kama watafikia makubaliano kuna uwezekano Noadia kutimkia moja ya timu hizo.
"Kuna timu kadhaa zinamhitaji, Mashujaa wameonyesha nia ya kumtaka lakini JKT wanaonekana kuwa na ofa nzuri zaidi, kwa sasa wanaendelea kufuatilia kila hatua kwa sababu wanaamini anaweza kuwasaidia msimu ujao," kilisema chanzo hicho.
Ushindani umeanza kuonekana mapema kwenye usajili kabla hata ligi yenyewe haijaanza na inaelezwa Alliance wanahitaji pesa tu kumuachia Noadia ambaye ameonekana kuwa lulu dirisha hili.
Noadia alikuwa mmoja wa nyota walionyesha kiwango bora Ligi Kuu ya Wanawake msimu uliopita baada ya kufunga mabao saba, rekodi iliyomfanya kuwa kiungo mshambuliaji aliyefunga mabao mengi zaidi msimu uliopita.
Uwezo wake wa kucheza nyuma ya mshambuliaji, kutengeneza nafasi na kufunga umemfanya kuwa mmoja wa wachezaji adimu kwenye soko la usajili.
Kwa Alliance Girls, huu unaweza kuwa wakati wa kufanya uamuzi wenye manufaa kwa pande zote mbili. Klabu hiyo inaweza kunufaika kifedha kupitia uhamisho huo, huku Noadia akipata jukwaa kubwa zaidi la kuendeleza kipaji chake katika timu yenye malengo makubwa ya ushindani wa ndani na kimataifa.