Waendesha baiskeli 100 kukiwasha Arusha
Arusha. Zaidi ya waendesha baiskeli 100 mkoani Arusha wanatarajiwa kushiriki katika mashindano ya baiskeli yatakayofanyikwa Aprili 22 jijini hapa.
Akizungumzia mashindano hayo, Muandaaji wa mbio hizo za baiskeli, Linus Katabalo amesema kuwa, lengo la mashindano hayo ni kumpongeza Nabii Mkuu GeorDavie kwa kazi kubwa anayoifanya ya kusaidia jamii katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
"Tumeamua kuandaa mashindano haya kwa lengo la kumpongeza Nabii Mkuu kwa namna ambavyo anasaidia jamii pamoja na kusaidia vijana bila kujali kabila wala dini hilo ni jambo kubwa na linahitaji kupongezwa na kuungwa mkono kwani ni watu wachache wenye moyo huo," amesema Linus.
Amesema mashindano hayo yataanzia barabara ya Haki iliyopo Kisongo na kutumia kilometa 45 baada ya mashindano hayo washindi mbalimbali watapatiwa zawadi.
Aidha ameongeza kama vijana wanatambua na kudhamini mchango mkubwa ambao unaofanywa na Nabii Mkuu kwa jamii inayomzunguka hivyo hawana budi kushirikiana naye na kuendelea kumuunga mkono kwa juhudi zake hizo.
Kwa upande wa waendesha baiskeli hao, Mohamed amesema jambo linalofanywa na Nabii Mkuu GeorDavie ni jambo kubwa sana kwani anasaidia watu kujikwamua kiuchumi na kuondokana na changamoto mbalimbali za maisha jambo ambalo ni kubwa sana na linahitaji kupongezwa na kuungwa mkono kwa kiwango cha juu.
Mwendesha baiskeli mwingine Ezekiel Mwakyoma amewataka vijana wengine kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano hayo.