Gamondi afunguka mchakato kumpata mrithi wa Samatta Stars
Muktasari:
- Hatua hiyo inakuja kufuatia Samatta kuweka ngumu juu ya maombi ya kubadilisha uamuzi wake wa kustaafu kuitumikia Taifa Stars, baada ya serikali kupitia Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Gamondi kujaribu kwa nyakati tofauti kumtaka mshambuliaji huyo kubadilisha uamuzi wake.
WAKATI kikosi cha Taifa Stars kikiendelea na maandalizi ya mchezo wake wa kwanza kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2027) dhidi ya Guinea Bissau, kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi amefunguka juu ya mchakato wa kumpata mrithi wa nahodha, Mbwana Samatta.
Hatua hiyo inakuja kufuatia Samatta kuweka ngumu juu ya maombi ya kubadilisha uamuzi wake wa kustaafu kuitumikia Taifa Stars, baada ya serikali kupitia Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Gamondi kujaribu kwa nyakati tofauti kumtaka mshambuliaji huyo kubadilisha uamuzi wake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi amesema baada ya hesabu za ushawishi kwa Samatta kukwama, ameshaanza mchakato wa kumpata mrithi wa mshambuliaji huyo aliyeitumikia timu ya Taifa kwa miaka 15.
Gamondi amesema tayari ameshapata majina ya wachezaji watatu ambayo moja kati ya hayo anaweza kuwa nahodha mpya lakini akiwaachia wachezaji wa kikosi hicho kufanya uamuzi wa mwisho.
Kocha huyo amewataja wachezaji hao watatu ambao mmoja kati yao atakuwa nahodha mpya ni beki Bakari Mwamnyeto ambaye pia ni nahodha wa Yanga, mshambuliaji Simon Msuva na kiungo Novatus Dismas.
"Tayari tumeshaanza huo mchakato, tulijitahidi kwanza kubadilisha msimamo wa Samatta lakini bahati mbaya inaonekana ametoa nafasi kwa wachezaji wengine kuendelea kuitumikia timu ya Taifa," amesema Gamondi.
"Tunalazimika kukubaliana na uamuzi wake lakini hapo hapo tukitafuta nani atakuja kuwa mrithi wake, kama kocha nina mawazo yangu kuna majina matatu nayafikiria.
"Mpaka sasa nina Bakari Mwamnyeto ambaye wote tunafahamu namna nafasi yake ilivyo kwenye timu lakini pia kuna Novatus, ukimtazama unaona anaweza sio kwasasa tu mpaka baadaye kulingana na umri wake, pia yupo Simon ni mchezaji ambaye amekuwa na nafasi yake.
"Sitaki kufanya uamuzi peke yangu, nimepanga kuwapa wachezaji wenyewe nafasi ili wamchague nani anafaa katika watu hao ili awe kiongozi wao kiwanjani na nje ya uwanja.
"Ninachotaka ni kuona tunapata mtu sahihi awe na nidhamu kubwa na awe kiongozi wa kweli uwanjani kuwasaidia wenzake, hilo ndio muhimu."
Hata hivyo, wakati Gamondi akiyaweka wazi hayo, uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini kuwa Mwamnyeto na Msuva mmoja wao ana nafasi kubwa ya kuwa nahodha mpya wa Stars.
Mwamnyeto anabebwa na rekodi yake ya kuwahi kuwa nahodha wa kikosi hicho kabla ya Samatta huku Msuva akibebwa na rekodi yake na nidhamu kwa wenzake.