Vipigo vyamvuruga Ibenge Azam
Muktasari:
- Kipigo hicho kinakuja baada ya Azam kuchapwa mabao 4-2 na Singida Black Stars katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, matokeo yanayoifanya timu hiyo kuingia katika kipindi kigumu huku maswali yakianza kuongezeka kuhusu uimara wa kikosi hicho.
KOCHA wa Azam FC, Florent Ibenge, anakabiliwa na kazi ya kurejesha utulivu ndani ya kikosi chake baada ya timu hiyo kupoteza mechi mbili mfululizo, ikiwamo kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kipigo hicho kinakuja baada ya Azam kuchapwa mabao 4-2 na Singida Black Stars katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, matokeo yanayoifanya timu hiyo kuingia katika kipindi kigumu huku maswali yakianza kuongezeka kuhusu uimara wa kikosi hicho.
Katika michezo hiyo miwili, changamoto zinazoonekana kuhitaji kupatiwa ufumbuzi na Ibenge ni uimara wa safu ya ulinzi, namna mabeki wanavyoshirikiana na matumizi ya nafasi za kufunga mabao.
Dhidi ya Al Ahli Tripoli, Azam ilionekana kuwa na udhaifu katika namna ilivyokuwa ikizuia mashambulizi ya wapinzani, hasa pale ilipokuwa imepeleka wachezaji wengi mbele kutafuta mabao na kuacha nafasi nyuma.
"Nafikiri dhidi ya Al Ahli Tripoli tulikuwa bora zaidi kuliko tulivyokuwa katika mechi yetu ya ligi. Tumepoteza na ni matokeo mabaya kwetu, lakini hatuna sababu ya kutazama chini vichwa vyetu. Tunatakiwa kuangalia mbele huku tukijiimarisha," alisema Ibenge.
Pamoja na mabao mawili iliyoruhusu, Azam ilimiliki mpira kwa asilimia 67 dhidi ya 33 za Al Ahli Tripoli na kupiga mashuti 17, manne yakilenga lango. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa timu hiyo iliweza kutengeneza mashambulizi, lakini ilikosa ufanisi wa kutosha katika eneo la mwisho.
Kwa Ibenge, changamoto sasa ni kuhakikisha uwezo wa timu katika kumiliki mpira na kushambulia unaambatana na nidhamu ya kulinda lango. Vilevile, anahitaji kurejesha makali ya safu ya ushambuliaji ili nafasi zinazotengenezwa zizae matunda.
Vipigo hivyo viwili mfululizo vinaifanya Azam kuwa na jukumu la kurekebisha makosa mapema, hasa ikizingatiwa kuwa inashiriki mashindano ya ndani na kimataifa yenye ushindani mkubwa.