Dickson Job: Kila mechi sasa ni fainali
Muktasari:
- Job amesema hayo baada ya Yanga kuanza vibaya hatua ya makundi kwa kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya MC Alger katika mchezo uliofanyika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ambapo bao la Soufiane Bayazid dakika ya 90 liliamua matokeo hayo.
NAHODHA wa Yanga, Dickson Job, amesema kikosi hicho kitalazimika kuichukulia kila mechi iliyobaki katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama fainali ili kuhakikisha kinapata pointi muhimu za kufuzu hatua ya robo fainali.
Job amesema hayo baada ya Yanga kuanza vibaya hatua ya makundi kwa kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya MC Alger katika mchezo uliofanyika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ambapo bao la Soufiane Bayazid dakika ya 90 liliamua matokeo hayo.
Job anasema kupoteza mchezo wa kwanza si jambo zuri, lakini matokeo hayo yamekuwa kama tahadhari kwao na sasa wanapaswa kuinua vichwa na kuelekeza nguvu kwenye michezo inayofuata.
“Si kitu kizuri kupoteza mchezo wa kwanza, lakini tunachoshukuru ni kwamba mchezo huu umetustua na kutuonyesha kuwa tunahitaji kuinua vichwa vyetu na kuangalia tunakwenda wapi. Nafasi bado ipo kwa sababu ndiyo kwanza mchezo wa kwanza, kwa hiyo kila mchezo uliopo mbele yetu sasa ni fainali,” amesema Job.
Nahodha huyo amekiri mchezo dhidi ya MC Alger ulikuwa mgumu huku akieleza kuwa walijitahidi kushambulia na kutafuta mabao lakini wapinzani wao walijilinda vizuri na kuwafanya washindwe kupata matokeo waliyokuwa wakiyahitaji.
Amesema kilichowagharimu zaidi ni kupoteza umakini katika dakika za mwisho, hali iliyowapa MC Alger nafasi ya kupata bao lililoamua mchezo huo kupitia mpira wa kutenga.
“Ulikuwa mchezo mgumu na tulijitahidi kuwapush ili tuweze kupata mabao lakini waliweza kujilinda vizuri. Dakika za mwisho tukakosa umakini na ndiyo maana tukaruhusu bao la mpira wa kutenga,” amesema.
Job amesisitiza kuwa pamoja na matokeo hayo, nafasi ya Yanga kufuzu robo fainali bado ipo lakini wanatambua umuhimu wa kupambana kupata pointi tatu katika kila mchezo unaofuata ili kurejesha matumaini ya kusonga mbele.