Uwanja wa Fumba wafikia asilimia 87
Muktasari:
- Uwanja huo ni miongoni mwa miundombinu ya michezo inayotarajiwa kutumika katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, itakayofanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Kenya na Uganda.
WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dk Riziki Pembe Juma, amesema wizara hiyo itaendelea kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa Fumba ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Dk Pembe amesema hayo wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo uliopo Fumba, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Uwanja huo ni miongoni mwa miundombinu ya michezo inayotarajiwa kutumika katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, itakayofanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Kenya na Uganda.
Amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa uwanja huo na kuwahakikishia wananchi pamoja na wadau wa michezo kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati.
Alibainisha kuwa ujenzi umefikia asilimia 87, hatua inayoonesha maendeleo makubwa yaliyopatikana na kutoa taswira halisi ya uwanja huo unaotarajiwa kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya AFCON 2027.
“Viti 2,000 vimeanza kufungwa katika majukwaa ya uwanja. Pia, kazi za ujenzi wa miundombinu ya nje zinaendelea, ikiwemo viwanja vya mazoezi na vyumba vya wageni mashuhuri (VVIP),” amesema.
Kwa upande wake, Mshauri Elekezi kutoka Kampuni ya Alhitmy, Abdulhamid Omar, amesema maendeleo yaliyofikiwa ni mazuri na kwamba wanaendelea kufanya juhudi kuhakikisha uwanja huo unakamilika kwa wakati.
Ameongeza kuwa, wanatarajia kufikia asilimia 90 ya utekelezaji wa kazi za uwekaji wa viti na uboreshaji wa mazingira ya nje ya uwanja ifikapo Novemba mwaka huu.
Uwanja huo unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 36,500, huku hadi sasa viti 2,000 vikiwa vimefungwa.