Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usiku mmoja kabla ya mechi ya Mbwana Samatta

Muktasari:

Juzi usiku, nilikuwa na Samatta katika chakula cha jioni. Maisha ya hapa ni tofauti zaidi. Kila mchezaji anakaa kwake usiku mmoja kabla ya mechi. Tena ni mechi muhimu. Jana katika siku ya pambano kila mchezaji ametokea kwake, tena saa nane wakati mechi yenyewe inachezwa saa kumi na mbili.


Nipo Genk Ubelgiji na jana usiku kina Mbwana Samatta na kikosi kizima cha Genk walikuwa uwanjani kukipiga na klabu ya Oostende, pambano la Ligi Kuu ya Ubelgiji. Maisha yapo tofauti sana kati yao na sisi na ni wakati wa kutafakari.

Juzi usiku, nilikuwa na Samatta katika chakula cha jioni. Maisha ya hapa ni tofauti zaidi. Kila mchezaji anakaa kwake usiku mmoja kabla ya mechi. Tena ni mechi muhimu. Jana katika siku ya pambano kila mchezaji ametokea kwake, tena saa nane wakati mechi yenyewe inachezwa saa kumi na mbili.

Haya ndio maisha ya wenzetu. Wachezaji wanakutana saa nne tu kabla ya mechi. Kila mmoja anatokea nyumbani kwake. Hakuna anayekufuatilia, lakini kiwango chako uwanjani ndicho kitakachoamua hatima yako.

Katika soka letu kuna mambo mawili. Ukimuachia mchezaji basi atakachofanya ni kwenda baa, kuchukua mwanamke na kulala naye mpaka saa nne asubuhi. Lakini pia hata kama mchezaji hana mpango huo, bado viongozi wa timu yake wanaweza kuchukua simu yake na kuondoka nayo.

Kuifanya hali ya Ulaya ihamie Tanzania tunahitaji miaka mingi sana. Lakini huu ni wakati wa kuanza kuwanyoosha wachezaji wetu. Wengi kati yao wanaishi kwa sababu ya mpira. Hawajasoma sana shule na hakuna kazi wanazoweza kufanya nje ya soka. Kwa nini bado tunawachunga kama watoto wadogo.

Wanalipwa mamilioni ya pesa na klabu zetu, hasa zile kubwa. Hata hivyo, bado klabu zinapata wakati mgumu kuwachunga na kuwabembeleza kama watoto wadogo. Kwa nini hasa? Kuna kitu lazima kifanyike.

Kitu hiki lazima kianzie katika kufumua mfumo mzima wa mchezo wa soka nchini na kutengeneza wanasoka ambao wanajitambua. Nimegundua pia kuwa itatuchukua muda sana kupata mafanikio kama tunaendelea kutengeneza wanasoka mastaa wanaochungwa. Wanasoka mastaa wanaoishi katika mfumo wa kujitambua kama wa Samatta ndio ambao wanaweza kutupeleka kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Lakini pia lazima tuondoe mfumo wa kutuletea viongozi ambao wanasimama katika lawama ya uwepo wa tabia hii ya kuchunga wachezaji. Hawa ni viongozi ambao wamezoea kuhonga wachezaji wa timu pinzani. Kwa staili hii haamini kama mchezaji wake anaweza asihongwe. Huku akiwa anamlinda mchezaji wake asihongwe kwa kumchunga kambini, bado na yeye anazurura usiku kucha akipiga simu za wachezaji wa timu pinzani.

Tukitengeneza soka la kulipwa lenye mifumo, tutaondokana na tabia hii. Kila mtu atatambua wajibu wake, atakula kwa jasho lake, ataishi kwa jasho lake na ataheshimu kazi yake. Mwisho wa siku, ubora ndio ambao unaamua mechi.

Licha ya kuachwa huru mpaka saa nne kabla ya mechi kuanza, juzi na jana akili ya Samatta ilikuwa ni namna ambavyo angeweza kuipora nafasi ya mshambuliaji mwenzake mpya wa klabu hiyo, Nikos Karelis ambaye alinunuliwa kabla yake na amekuwa akifanya vema.

Kwa staili hii hauwezi kwenda baa usiku mmoja kabla ya mechi, na wala hauwezi kulala na mwanamke. Unahitaji kumpora mtu namba ili ufunge mabao mengi na kuuzwa kwingine na kupata mshahara mkubwa zaidi. Ni kitu cha kawaida katika soka la kulipwa kwa sababu soka ni maisha yako.

Vijana wetu tangu wakiwa wadogo tuwatengenezee mioyo ya kushindani na wajue kuwa wanaishi kwa ajili ya mpira au michezo ambao wanashiriki. Tatizo kubwa kwetu wachezaji hawashindani. Wakishaingia katika kikosi cha kwanza wanacheza kwa ajili ya majina yao.

Kama wangekuwa wanashindana wala kusingekuwa na haja ya kuwachunga kwa kuhofia kuwa watahongwa au kufanya vitendo visivyofaa usiku mmoja kabla ya mechi. 

Kama ilivyo kwa mwanasheria, daktari, mwalimu, mwandishi wa habari, mhandisi na watu wengine wa fani mbalimbali, mbona wao hawalali kambini siku moja kabla ya kwenda kazini au semina? 

Wanatambua muda wanaotakiwa kufika kazini na wanatambua umuhimu wa kuwa na ufanisi katika kazi.

Soka ni ajira kama hizi ajira nyingine. Sasa hivi kuna wanasoka wengi nchini wanaolipwa mshahara na kupata kipato ambacho asilimia 80 ya Watanzania hawakipati. Kwa nini tuwachunge? Utengenezwe mfumo kuwa asipoifanya kazi yake kwa ufasaha, basi mtu mwingine atapewa nafasi yake. Labda kama anashindwa kuifanya kazi hiyo kwa sababu za kibinadamu kama maradhi au matatizo ya kisaikolojia. Vinginevyo kwa nini abembelezwe?