Unaikumbuka ile Simba iliyopindua?
UNAUKUMBUKA zaidi mchezo upi wa watani wa jadi Simba na Yanga? Ni mchezo gani ulikusisimua na kukuburudisha zaidi? Bila shaka ipo kadhaa.
Ukizungumza na Wahenga (watu wa kale) watakwambia kuwa wanaukumbuka zaidi mchezo wa mwaka 1977 ambao ulimalizika kwa Simba kuifunga Yanga mabao 6-0. Haijawahi kutokea tena mpaka leo.
Mchezo huo umeendelea kuwa wa kihistoria kutokana na ukweli kwamba ndiyo mtanange pekee wa watani wa jadi ambao ulishuhudia mchezaji mmoja akifunga mabao matatu ‘hat trick’. Alikuwa ni Abdallah ‘King’ Kibadeni, ambaye kwa sasa ni mzee.
Kwa kifupi ipo michezo mingi ya watani wa jadi ambayo unaweza kuikumbuka kutokana na sababu fulani. Yawezekana ni kutokana na mabao yaliyofungwa. Yawezekana ni kutokana na kadi nyekundu zilizotawala. Pia inawezekana ni kutokana na ukali wa mchezo wenyewe. Sababu ziko nyingi.
Makala haya yanatazama mechi kali zaidi za watani wa jadi katika kipindi cha miaka 10 tu iliyopita. Ni ipi ilivutia zaidi?
Simba 3-3 Yanga, Oktoba 2013
Kuna mchezo gani mkali wa watani wa jadi zaidi ya huu? Mchezo huo ulipigwa Oktoba 20, 2013 na kuacha historia ya kipekee. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Yanga ilikuwa mbele kwa mabao matatu yaliyofungwa na Hamis Kiiza (mawili) na Mrisho Ngassa. Kila mtu aliamini kuwa Simba ingefungwa mabao zaidi kipindi cha pili.
La haula! Simba ikapindua mambo kabisa kipindi cha pili. Simba ilirejea uwanjani kama Mbogo aliyejeruhiwa. Ililisakama lango la Yanga kama haina akili nzuri. Matokeo ya mwisho yaliwashangaza wengi kwani Simba ilifanikiwa kukomboa mabao yote matatu. Watu zaidi ya 20 walipoteza fahamu kwa jinsi Betram Mombeki, Joseph Owino na Gilbert Kazze walivyopindua matokeo kiaina.
Simba 2-1 Yanga, Februari 2017
Mchezo huu uliopigwa mapema mwaka huu, nao uliwaacha watu midomo wazi. Matokeo ya mwisho ndio yalikuwa ya kushangaza zaidi. Katika mchezo huo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Yanga ilikuwa mbele kwa bao 1-0. Lilikuwa bao la mapema la Saimon Msuva kwa mkwaju wa penalti.
Wakati Simba ikipambana kukomboa bao hilo, ilipata pigo kwa beki wake Janvier Besala Bokungu kuonyeshwa kadi nyekundu. Jahazi la Simba lilionekana kuzama, tena katika eneo korofi la Nungwi.
Mambo yaligeuka ghafla. Simba ilianza kutandaza soka la kuvutia. Yanga ikautafuta mpira kwa tochi. Laudit Mavugo akafunga bao la kusawazisha kabla ya Shiza Kichuya kufunga bao la ushindi ambalo ndilo lilitangazwa kuwa bao bora la msimu. Kwa mtu aliyekuwa anautazama mchezo kwa mbali, angedhani Yanga ndiyo ilikuwa pungufu. Aibu iliyoje.
Simba 4-3 Yanga, April 2010
Mechi nyingine kali ya watani ilichezwa mwaka 2010. Simba ilikuwa tayari imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na mchezo huo ulikuwa ni wa heshima tu. Soka lilipigwa sana. Simba iliyokuwa na rekodi ya kutopoteza mchezo msimu huo ilicheza soka la maana.
Mabao mawili ya Mussa Hassan Mgosi na mengine mawili kutoka kwa Uhuru Seleman na Hillary Echesa yalitosha kuilaza Yanga mapema. Katika mechi hiyo ya funga nikufunge, Yanga ilipata mabao yake matatu kupigia kwa Jerryson Tegete (mawili) na Athuman Idd ‘Chuji’. Hata hivyo mwamuzi wa mchezo huo alifungiwa kwa kuiminya Yanga.
Yanga 1-0 Simba, Oktoba 2008
Baada ya utawala wa Simba wa miaka nane mfululizo, Yanga ilifanikiwa kuvunja mwiko mwaka 2008 kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0. Yanga ilikuwa imecheza dhidi ya Simba kwa miaka yote hiyo mfululizo bila ushindi wowote katika mechi za Ligi Kuu.
Kikosi cha mwaka 2008 kilibadili upepo. Wakati huo mastaa wa Yanga waliongozwa na Ben Mwalala, Godfrey Bonny (marehemu) Boniface Ambani, Mrisho Ngassa na Juma Kaseja. Mwalala ndiye aliyepeleka furaha Jangwani baada ya kufunga bao pekee la ushindi.
Simba 5-0 Yanga, Mei 2012
Unaweza kusema hii siyo mechi kali kwa kuwa ilikuwa ya upande mmoja zaidi. Nani kakudanganya? Hii ni mechi ya kihistoria. Kwa mechi za watani, timu moja kufungwa mabao 5-0 siyo jambo jepesi hata kidogo. Hili liliikuta Yanga mwaka 2012 na mpaka leo aibu hiyo inawaandama.
Hii ndiyo mechi iliyompa heshima Emmanuel Okwi aliyefunga mabao mawili. Mpaka leo watu wa Simba wanampenda Okwi kuliko hata wanavyoipenda timu yao. Mabao mengine yalifungwa na Patrick Mafisango (marehemu), Juma Kaseja na Felix Sunzu.
Simba 1-0 Yanga, 2007
Mechi nyingine kali hii hapa, ilipigwa pale Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri. Wakati huo Yanga ilikuwa ikipokea noti za kutosha kutoka kwa aliyekuwa mfadhili wao, Yusuf Manji lakini mambo hayakuwa mazuri kwao.
Simba ilipata pigo katika dakika ya 15 tu baada ya Henry Joseph kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Othman Kazi. Hata hivyo furaha bado ilikwenda Msimbazi. Ulimboka Mwakingwe aliifungia Simba bao pekee la ushindi katika dakika ya 30. Pamoja na mapambano yote, Yanga waliondoka uwanjani vichwa chini lakini hasira zao walizimalizia kwa kipa Ivo Mapunda na beki, Shadrack Nsajigwa kwa madai kuwa wamefungisha!