Uchaguzi Yanga: Mwakyembe uso kwa uso kamati ya uchaguzi TFF
Muktasari:
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe anategemea kesho kupata taarifa kuhusu mchakato wa Uchaguzi mkuu wa Yanga na kujadili changamoto zilizopo na kuzitatua.
Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kesho anatarajia kupokea taarifa kuhusu mchakato wa uchaguzi mkuu wa Yanga unaotarajia kufanyika Januari 13 mwakani.
Uchaguzi huo umeonekana kuwa na utata mkubwa kwani pande mbili zinavutana, Yanga ikitaka uchaguzi huo usimamiwe na kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kamati yake ya uchaguzi tayari inaendelea na mchakato wa uchaguzi.
Jambo ambalo linaleta mgogoro katika suala hilo ni Yanga kuendelea kumtambua Yusuph Manji kama mwenyekiti wao na kutaka kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi nyingine tu na si ya mwenyekiti wakati TFF ikiwataka kufanya uchaguzi wa nafasi zote ikiwemo ya mwenyekiti.
Licha ya Kamati ya Utendaji ya Yanga na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kukutana wiki iliyopita, lakini bado hawakufikia muafaka huku mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Malangwe Mchungahela akishikilia msimamo kuwa uchaguzi huo utasimamiwa na kamati hiyo na hawamtambui Manji kama mwenyekiti wa Yanga
Mwakyembe alisema kesho Jumatano wakati akikutana na Kamati ya maandalizi ya mashindano ya Afcon kwa vijana chini ya miaka 17, yatakayofanyika mwakani hapa nchini pia atapewa taarifa kuhusu maendeleo ya mchakato wa uchaguzi wa Yanga.
"Mimi huwa sitaki kusikia mambo ya barabarani nataka vitu viwekwe mezani ili kama kuna changamoto tuitatue.
"Mpaka sasa bado hawajaniletea taarifa na kesho kabla ya kikao cha Afcon nina uhakika watanipa taarifa kuhusu mchakato wa uchaguzi ili kama kuna changamoto ziweze kutatuliwa."
"Sidhani kama suala la Yanga ni gumu ni jambo la kutumia hekima na busara ili tuweze kusonga mbele," alisema Mwakyembe
Tayari Kamati ya uchaguzi ya TFF imewafanyia usaili wagombea na kupitisha majina 22 ya wanaowania uongozi wa nafasi mbalimbali Yanga.
Katika nafasi ya mwenyekiti wapo Dk.Jonas Tiboroha, Mbaraka Igangula na Erick Ninga wakati nafasi ya makamu mwenyekiti ni Yono Kevela, Titus Osoro na Salum Chota.
Wajumbe waliopitishwa ni Salim Seif, Hamad Ally, Shafil Amri Islam, Benjamin Mwakasonda, Sylvestre Haule, Said Kambi, Dominick Francis, Seko Jihadhari, Ally Omar Msigwa, Arafat Hajji, Frank Kalokola, Ramadhani Said, Leonard Marango, Bernard Mabula, Christopher Kashiririka na Athanas Kazige.