Uchaguzi Simba, watatu watinga kuchukua fomu
Muktasari:
- Kakayoo amechukua fomu hiyo jana, Novemba 18, 2026, akiungana na wanachama wengine waliojitokeza katika zoezi la kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya klabu hiyo.
MWANACHAMA wa Klabu ya Simba, Hassan Bakari Kakayoo maarufu kama Mzee wa Salute, na wengine wawili walichukua fomu ya kuwania nafasi ya ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, akieleza kuwa kufanya hivyo ni haki yake ya msingi ya kikatiba.
Kakayoo amechukua fomu hiyo jana, Novemba 18, 2026, akiungana na wanachama wengine waliojitokeza katika zoezi la kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya klabu hiyo.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Kakayoo amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kufika salama na kutimiza hatua hiyo katika mchakato wa uchaguzi wa Simba.
“Nimeweza kuchukua fomu hii kwa sababu ni haki yangu ya msingi ya kikatiba. Lakini kutokana na miongozo mbalimbali ya utaratibu, kuna baadhi ya vitu ambavyo kwa sasa siwezi kuvizungumzia,” alisema Kakayoo.
Alifafanua kuwa hii si mara yake ya kwanza kuingia katika mchakato wa kuwania nafasi ya ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, kwani aliwahi kuchukua fomu kama hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2022.
Tofauti hiyo imeonekana jana, ambapo idadi ya watu waliojitokeza katika eneo la ofisi hizo ilikuwa ndogo ikilinganishwa na siku zilizopita, ambazo zilishuhudia vigogo mbalimbali wa Simba wakifika kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi, pia Wilfred Nyamwija naye ameingia kwenye mchakato huo kwa kuwania nafasi ya ujumbe ndani ya klabu hiyo.
Jina jingine lililojitokeza jana ni Salum Hamidu, Makamu Mwenyekiti wa Matawi ya Simba jijini Dar es Salaam, ambaye pia alifika kuchukua fomu huku akigoma kuzungumza lolote.
Kujitokeza kwa Nyamwija na Hamidu kumefanya jana watu watatu pekee wawe wamechukua fomu hadi kufika saa 10:00 jioni.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Januari 30, 2027, badala ya Januari 3 kama ilivyokuwa imepangwa awali. Viongozi watakaopatikana wanatarajiwa kupokea kijiti kutoka kwa uongozi unaomaliza muda wake chini ya Mwenyekiti Murtaza Ally Mangungu.