Twiga Stars ipo tayari kwa WAFCON 2026
Muktasari:
- WAFCON itakayoanza Julai 26, hadi Agosti 16, 2026 nchini Morocco, kwa Twiga Stars itakuwa ni mara ya tatu inashiriki baada ya mwaka 2010 na 2024 kuishia makundi.
KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania, Twiga Stars Bakari Shime amesema maandalizi ya kikosi chake kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 yanaendelea vizuri na mechi za kirafiki walizopanga kucheza nchini Morocco zitawapa picha halisi ya kiwango cha timu kabla ya kuanza mashindano.
Shime amesema Twiga Stars inatarajia kucheza mechi mbili za kimataifa za majaribio katika mji wa Rabat, ili kupima utayari wa kikosi chake kabla ya mchezo wa kwanza wa Kundi B dhidi ya Afrika Kusini.
Amefafanua, Julai 19 watacheza dhidi ya Nigeria, kabla ya Julai 22 kukutana na mshindi kati ya Ghana na Mali.
“Malengo ya mechi hizi ni kuona yale ambayo tumeyafanyia kazi kwa takribani wiki tatu. Tunataka kujua ni maeneo gani tumefanya vizuri na ni sehemu zipi bado zinahitaji maboresho kabla ya mchezo wetu wa kwanza dhidi ya Afrika Kusini tarehe 27,” amesema Shime.
Kocha huyo amesema moja ya mambo makubwa yaliyowakwamisha katika WAFCON iliyopita ilikuwa ni wimbi la majeruhi kwa baadhi ya wachezaji muhimu pamoja na uchovu uliotokana na ratiba ngumu ya mashindano.
Amesema Twiga Stars ilipoteza nguvu baada ya baadhi ya nyota wake kupata majeraha wakiwa tayari kwenye mashindano, huku wengine wakikabiliwa na adhabu za kadi walizopewa kwenye mechi za kufuzu.
“Ufanisi wa baadhi ya wachezaji haukuwa mzuri kutokana na majeraha. Pia tulikuwa na changamoto ya kadi tulizoingia nazo kutoka mechi za kufuzu, lakini vilevile tulikuwa na muda mfupi wa maandalizi ukilinganishwa na safari hii,” amesema.
Shime amesema safari hii maandalizi yamekuwa bora zaidi na benchi la ufundi limejipanga kuhakikisha changamoto hizo hazijirudii.
Amebainisha kuwa licha ya kuwepo kwa baadhi ya majeraha madogo, idara ya tiba inaendelea kufanya kazi kuhakikisha wachezaji wote wanarejea kwenye utimamu kwa asilimia mia moja kabla ya mashindano kuanza.
“Sasa hivi tuna majeraha machache, lakini tunaendelea kupambana kuhakikisha kila mchezaji anakuwa tayari kwa ajili ya mashindano,” amesema.
Kocha huyo pia amepongeza Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kufanya maboresho kwenye ratiba ya mashindano, akisema yatawasaidia wachezaji kupata muda wa kutosha wa kupumzika kati ya mechi.
Amesema tofauti na toleo lililopita ambapo timu zilikuwa zinacheza karibu kila baada ya siku moja, safari hii muda kati ya mchezo mmoja na mwingine umeongezwa, jambo litakalosaidia kupunguza uchovu wa wachezaji.
Mbali na hilo, Shime amesema CAF imeongeza idadi ya wachezaji wanaoruhusiwa kusajiliwa kwenye kikosi cha mashindano, hatua ambayo itazipa timu nafasi kubwa ya kufanya mabadiliko pale inapohitajika.
Amekumbusha pia kuwa katika WAFCON iliyopita Twiga Stars ililazimika kusafiri umbali mrefu kutoka kambini hadi viwanjani, hali iliyoongeza uchovu kwa wachezaji, lakini safari hii mazingira yanaonekana kuwa rafiki zaidi.
Twiga Stars ipo Kundi B pamoja na mabingwa watetezi Afrika Kusini, Ivory Coast na Burkina Faso, huku ikilenga kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia ya ushiriki wake kwenye mashindano hayo.
WAFCON itakayoanza Julai 26, hadi Agosti 16, 2026 nchini Morocco, kwa Twiga Stars itakuwa ni mara ya tatu inashiriki baada ya mwaka 2010 na 2024 kuishia makundi.