Timu za Ligi Kuu Bara kutumia viwanja vya Zanzibar

Muktasari:
- Kasongo ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari waliohudhuria semina inayoendeshwa na bodi hiyo.
MTENDAJI Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Almas Kasongo amesema kuanzia msimu ujao wa Ligi 2024/25, ni ruksa kwa timu ya Ligi Kuu Bara kutumia viwanja vya Zanzibar.
Kasongo amesema moja ya kanuni zilizofanyiwa maboresho kuelekea msimu mpya ni hiyo ya matumizi ya viwanja vya Zanzibar kwenye Ligi Kuu.
“Katikati ya msimu ofisi yangu illipokea ombi la timu ya Simba kwenda kutumia Uwanja wa New Amaan Complex kwa ajili ya Ligi Kuu, lakini haikuwezekana kwa sababu ya kanuni japo hoja zao zilikuwa na mashiko,” alisema.
“Tulikaa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na tukaona hakuna sababu ya kuzuia hilo lakini tukasema ni vyema kanuni hiyo ianze kutumika msimu ujao 2024/25,” alisema Kasongo.
Katika hatua nyingine, alisema ndani ya siku mbili mashabiki watafahamu ratiba ya Ligi Kuu Bara 2024/25 inayoanza baadaye mwezi huu.
“Ratiba ya ligi pamoja na maboresho ya kanuni zipo tayari na ndani ya siku hizi mbili ofisa habari wa ligi ataweka hadharani kila kitu.
“Ni kweli tulikuwa kimya kwa muda mrefu, lakini kimya kirefu kina mshindo, hivyo tunaamini ratiba ya msimu huu itakuwa bora,” alisema Kasongo.
Katika hatua nyingine alisema viwanja visivyo na uwezo wa kubeba watu 3,000 havitatumika msimu wa 2024/25 na uamuzi huo unalenga kuimarisha mazingira ya michezo kwa kuzingatia usalama na faraja ya mashabiki.
“Kiwanja ambacho hakitakuwa na jukwaa lenye uwezo kubeba wadau wa soka elfu tatu hakitatumika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara 2024/25 ili kulinda hadhi ya soka letu. Tunaamini kuweka kiwango hiki cha chini kutaboresha usalama na kuongeza mapato ya klabu kwa kuvutia mashabiki wengi, Bodi ya Ligi itashirikiana na klabu na wadau kuhakikisha miundombinu inaboreshwa ili kufikia viwango vinavyohitajika,” alisema.
Akizungumzia maboresho ya kanuni, Katibu Mkuu wa Coastal Union, Omar Ayoub alisema kucheza Zanzibar itakuwa jambo bora kuwahi kutokea upande wao kwa miaka ya hivi karibuni.
“Ni suala zuri na sisi kama Coastal Union tunalipokea kwa uzuri kwani tulikuwa Kisiwani Pemba kwa kambi ya muda tumekutana na viwanja bora na mazingira mazuri huko. Huenda na sisi tukachagua kuchezea huko kutokana na mazingira,” alisema.
“Kutoka Tanga hadi Pemba tunatumia saa moja na nusu na kutoka Pemba hadi Unguja saa moja na nusu, hivyo tunaweza kutumia saa mbili kwenda na kurudi, lakini safari ya Tanga kwenda Arusha ni zaidi ya saa tatu hadi nne.”
Alisema ni bora safari ya majini kuliko kutumia mabasi hivyo suala la kutumia viwanja vya Zanzibar ni jema zaidi kwao.
Msimu wa Ligi Kuu Bara 2024/25 unatarajiwa kuanza rasmi Agosti 16.